Baada ya mchezo wa raundi ya kwanza kumalizika kwa sare ya mabao mawili kwa mawili huku Simba waliokua nyumbani wakionekana kama wamepoteza baada ya Yanga Sc kufanya “comeback” ya nguvu ndani ya dakika tano sasa ni vita tena katika raundi ya pili huku Yanga akiwa mwenyeji.
Kuelekea mchezo huo tayari kuna wachezaji nyota katika kila timu ambao wanatarajiwa kufanya mambo makubwa katika “Derby” ya Kariakoo. Nyota kama Deo Kanda, Luis Miquissone, Cleotus Chama na Francis Kahata wamekua wakitegemewa na mashabiki wa Simba kuwapa furaha March 08. Lakini pia kwa upande wa Yanga Benard Morrison, Ditram Nchimbi, Haruna Niyonzima na David Molinga nao wapo katika kiwango kizuri kuelekea Derby hiyo.
Kuelekea mchezo huo tunakuletea wachezaji wanaotarajiwa kuanza na kukutana na upinzani wa hali ya juu siku ya mchezo huo. Miongoni mwa vita hizo ni hizi hapa:
Juma Abdul vs Francis Kahata.
Ni wazi kabisa wachezaji hawa watakua katika mpango wa walimu siku ya mchezo, uwezo mkubwa wa kuuchezea mpira, kasi na chenga ndio silaha kubwa ya Kahata ambae anakwenda kukutana na beki mzoefu ambae yuko vizuri kwasasa Juma Abdul. Miongoni mwa sehemu muhimu za mbinu katika mchezo huu ni maeneo ya pembezoni mwa uwanja.
Japhary Mohamed vs Deo Kanda.
Deo kanda anasifika kwa uwezo mkubwa wa kupiga chenga na kuwatoka mabeki wa timu pinzani lakini anakwenda kukutana na Japhary ambae kiasili ni kiungo na si beki wa pembeni. Upande wa kulia wa Simba na kushoto kwa Yanga unategemewa kua “busy” sana siku ya mchezo kutokana na uwezo wa wachezaji hao wanaotarajiwa kuanza katika maeneo yao.
Chama vs Niyonzima
Hapa ndipo burudani ya mchezo ulipo na hawa ndio watakaobeba mabomu kutokana na mbinu za walimu wa timu zote mbili. Viungo hawa mafundi watakutana katika eneo la katikati mwa uwanja huku kila mmoja akitaka kuchukua udhibiti wa eneo hilo. Chenga za maudhi, pasi za hatari na uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi za mabao ni vitu ambavyo wawili hawa wanavyo.
Katika vita hii ni kwa kiasi kikubwa inategemewa ndio itakayoamua mchezo. Kati ya Chama na Niyonzima atakaekua mshindi wa vita hii katikati ya uwanja huenda ndie atakaeipa ushindi timu yake.
Shomary Kapombe vs Benard Morrison
Benard Morrison kipenzi kipya cha Yanga akiwa na uwezo mkubwa wa kupiga chenga na kutengeneza nafasi na kufunga pia ndio muhimili mkubwa kwasasa katika kikosi cha Yanga. Uwezo wake katika kuwatesa walinzi wa timu pinzani huenda akawa kikwazo kikubwa kwa Kapombe ambae hupenda kupanda kushambulia kupitia upande wa kulia. Morrison nidie mshehereshaji mkubwa kwasasa haswa kwa mashabiki wa Yanga.
Ditram Nchimbi vs Hussein Tshabalala.
Nguvu, kasi na krosi tamu ndio silaha kubwa ya Nchimbi kwasasa haswa baada ya kuhamishwa kutoka kama mshambuliaji wa kati na kupelekwa kucheza pembeni. Nchimbi anakwenda kukutana na Tshabalala ambae hutumia akili nyingi huku akiwa na akili ya kushambulia zaidi kuliko kukaba.
Nchimbi pia huenda akatumika kama mshambuliaji wa kati na akakutana na Pascal Wawa pia katika eneo la ulinzi la Simba.
Luc Aymael vs Van Debroek
Wabelgiji hawa wanakwenda katika Derby wakiwa sawa kutokana na matokeo ya mwisho katika mchezo wa Ligi kupata ushindi.
Luc amekua akitumia mfumo wa 4:2:3:1 huku akiamini katika mpira wa pasi na kushambulia kwa kasi na kuwekeza katika viungo wake watatu Niyonzima, Mapinduzi na Tshishimbi eneo la kati na pia akitegemea kasi ya Morrison pembezoni mwa uwanja kuweza kupata ushindi.
Van Debroeck yeye ni muumini wa pasi nyingi na kwenda mbele kwa pasi za harakaharaka akipendelea kutumia mfumo wa 4:1:4:1. Katika mfumo huu Jonas Mkude amekua ndio kiunganishi muhimu cha timu akiianzisha timu ianze kucheza kutokea chini. Debroek amekua akiamini katika mashambulizi ya viungo wake wa pembeni Hassan Dilunga, Francis Kahata, Luis Miquissone na Deo Kanda.
Ama kwa hakika walimu hawa ndio watakaoamua mchezo kutokana na mbinu watakazozitumia na kuwapa wachezaji wao katika mchezo huo wa March 8.