Hii ni makala ya shabiki wa Yanga kutoka katika mitandao ya kijamii, tunaiwasilisha katika wakati huu Yanga ikisheherekea miaka 85 tangu kuanzishwa kwake.
Yanga leo inasherehekea miaka ya 85 ya kuzaliwa kwake, ambapo tukio maalum la maadhimisho ya kumbukumbu hiyo litafanyika baada ya mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mbeya City ambao utapigwa uwanja wa Taifa saa moja jioni
Historia ya Yanga
Ingawa historia inasema Yanga ilianzishwa mwaka 1935 na Simba mwaka 1936, lakini ukizama ndani utagundua kwamba , huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa utani na upinzani wa jadi baina ya miamba hiyo ya soka nchini.
Kulikuwa kuna timu inaitwa New Youngs ambayo mwaka 1936 ilisambaratika na baadhi ya wachezaji wake wakaenda kuunda timu iliyokuwa Sunderland, ambayo hivi sasa inajulikana kama Simba.
Kabla ya kutokea vurugu zilizoisambaratisha New Youngs vijana wa Dar es Salaam walikuwa na desturi ya kukutana viwanja wa jangwani kufanya mazoezi na baada ya muda wakaamua kuunda timu yao, waliyoipachika jina Jangwani Boys.
Ndani ya kipindi kifupi timu hiyo iliteka hisia za wengi, waliojitokeza kujiandikisha uanachama wa klabu hiyo, miongoni mwao waliovutiwa na uanachama wa klabu hiyo ni Tabu Mangala (Sasa marehemu) na ilipofika mwaka 1926 walifanya mkutano wa kwanza katika eneo ambalo hivi sasa kuna shule ya sekondari ya Tambaza.
Miongoni mwa yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo ni kuiboresha timu hiyo ambayo wachezaji wake wengi walikuwa wafanyakazi wa bandarini na mashabiki wake wengi walikuwa wabeba mizigo bandarini.
Baada ya mkutano huo, timu ilibadilishwa jina na kuwa Navigation, iliyotokea kuwa moto wa kuotea mbali katika timu za waafrika enzi hizo, kabla ya uhuru wa Tanganyika.
Timu kama Kisutu, Kitumbini, Gerezani na Mtendeni zilikuwa hazifui dafu kwa wana wa Jangwani hao.
Ikiwa inatamba kwa jina la Navigation, wanachama wa timu hiyo walikuwa wanatembea kifua mbele na kuwatambia wapinzani wao, kwamba katika kipindi hicho wao ndiyo zaidi, kwa sababu Italia ilikuwa inatamba kwenye ulimwengu wa soka, wanachama wa timu hiyo nao waliamua kuibadilisha jina timu yao na kuiita Italiana.
Taliana FC ilipata mafanikio ya haraka na haikushangaza ilipopanda ligi Daraja la pili kanda ya Dar es Salaam.
Mwanzoni mwa miaka ya 1930 Italiana waliamua kuachana nalo mapema kabla ya kuingia kwenye ligi hiyo, hivyo wakaanza kujiita New Youngs.
Kila kila ilipokuwa ikibadilisha jina, ilikuwa ikifanya vitu vipya pia, kwani wakiwa na jina la New Youngs waliweza kutwaa kombe la Kassum, lililoshirikisha timu mbalimbali za Dar es Salaam.
Hatimaye ukawadia mwaka mbaya kwa New Youngs 1936 wakati baadhi ya wachezaji walipojitoa na kwenda kuanzisha Sunderland.
Kwa sababu hiyo, waliobaki wakaamua kubadili jina na kuwa Young Africans jina ambalo mashabiki wake wengi walishindwa kulitamka vizuri hivyo kujikuta wakisema Yanga.
Miaka ya 85 baadaye leo, ni timu ya kihistoria Tanzania ikiwa inaongoza kutwaa ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara kwa mara 27.
Pongezi nyingi ziwaendee wachezaji wote waliopata kuichezea timu hiyo kuanzia enzi za Jangwani Boys, Navigation, Italiana, New Youngs hadi leo hii ikijulikana kama Yanga ingawa katika cheti chake cha usajili inafahamika kama Dar Young Africans.
Mafanikio ya Yanga ndani ya miaka 85 hayakuja hivi hivi bila kuwapongeza viongozi ambao waliihangaikia timu hiyo inasimama kidete, viongozi wa enzi hizo hadi leo hii wanastahili pongezi kwa kuiwezesha kutwaa mara nyingi ubingwa wa nchi.
Shukrani nyingine ziwaendee wanachama, wapenzi na mashabiki, bila kuwasahau waandishi wa habari, bila hamasa zao sidhani kama Yanga ingeweza kufika hapo ilipo, hiyo ndiiyo historia ya klabu ya Yanga ambayo ndio iliyozaa Sunderland leo hii ikiitwa Simba SC.
Nani angeijua Simba kama si Yanga? hivyo inajivunia ubora ilionao, Yanga imetoa viongozi mbalimbali wa soka na serikali mmoja wapo ni rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete ambaye mwaka 1976 alikuwa Mjumbe kamati ya usajili wa klabu hiyo na kuwezesha usajili wa Shaaban Katwila
HAPPY BIRTHDAY YANGA..! (Jina la Mwandishi bado kulipata)