Sifa yake kubwa ni kutembea juu ya mpira , sifa yake hatari ni kuisaidia timu kupata ushindi . Krosi zake ndiyo huwa mwanzo wa madhara kwenye timu pinzani.
Mechi tatu mpaka sasa hivi akiwa amevaa uzi wa njano na kijani , uzi ambao kimamlaka unamilikiwa na timu ya wananchi. Wananchi wenye mapenzi makubwa sana.
Wananchi ambao ni wafia timu haswa , timu ambayo ni kongwe na ni mabingwa wa muda mrefu wa ligi kuu ya Tanzania. Jina wapendao kuitwa ni jina la Yanga na mchezaji ambaye yuko mdomoni mwao kwa sasa ni Bernard Morrison.
Bernard Morrison ambaye jana alishikwa haswa kwenye mechi dhidi ya Mtibwa Sugar na kumfanya asiweze kufanya vyema kama alivyofanya kwenye mechi mbili zilizopita.
Kiongozi wa jeshi la zima moto aliyeongoza kuzima moto wa Bernard Morrison alikuwa Abdulhalim Humoud , kiungo katili wa Mtibwa Sugar.
Baada ya mchezo huo Abdulhalim Humoud alisema kuwa alipanga kutompa nafasi ya kupumua Bernard Morrison kwenye mechi ya jana.
“Sikutaka apate nafasi ya kuwa na mpira muda mrefu kwa sababu Bernard Morrison ni mchezaji mzuri sana ndiyo maana kila alipokuwa anashika mpira Mimi nilikuwepo kuhakikisha asiwe na nafasi ya kuwa na mpira”-alimalizia kwa kuweka wazi silaha alizotumia kuzima moto huo wa Bernard Morrison.