TIMU za Kaizer Chief na Orlando Pirates zimefanya usafi katika timu zao. Zimeacha ‘watumishi hewa’. Moja ya watumishi hao ni James Kotei ‘Iron Man’ aliyeachwa Kaizer Chief na ameamua kurudi kwao Ghana. Orlando Pirates wao wamemuacha mtumishi hewa Benard Morrison aliyeibukia Yanga na kuanza kukonga nyoyo.
Kuna kitu cha kuambiana hapa. Soka letu ni dhaifu. Inakuwaje Kotei aliyekuwa mwamba katika kiungo cha Simba msimu uliopita aonekane si lolote si chochote ndani ya Chief, huku Morrison akianza kujitengenezea maisha ya ufalme Jangwani wakati ameshindwa kutamba Pirates?
Soka letu limejaza wachezaji lele mama. Huu ni ukweli mchungu ambao watu wengi watagoma kuumeza. Haishangazi kuona Kotei anakuwa nyota mkubwa kwetu, lakini Afrika Kusini anakuwa mchezaji wa kawaida, huku Morrison akionekana mchezaji wa ajabu katika ardhi yetu.
Aliwahi kuniambia Seleman Matola alivyokwenda kucheza soka Afrika Kusini. Alisema “Mkeyenge mdogo wangu Afrika Kusini sio rahisi mtu kuwa staa. Aliendelea nilivyokuwa Simba mazoezi yote yaliyokuwa yakitolewa nilikuwa mstari wa mbele kuyafanya, hii ilinifanya baadhi ya wachezaji wenzangu wanione nataka sifa katika kufanya mazoezi, lakini hali ilikuwa tofauti nilivyokuwa Afrika Kusini.
Alinieleza kuwa “Nilijishangaa sana, sikujua kwanini imekuwa vile, lakini kiufupi ni kwamba wenzetu ni tofauti na sisi. Akamalizia kwamba hata “Nilivyorudi nyumbani niliwaongoza tena wenzangu katika mazoezi tuliyokuwa tunafanya.
Kuna wigo mrefu uko kwa wachezaji wanaocheza ligi yetu dhidi ya wachezaji wa ligi nyingine. Ndani ya Simba Kotei alikuwa mwanaume kweli kweli. Hata kuondoka kwake, kuliwaudhi manazi wa Simba walioamini bado alikuwa na kitu cha kuipa timu, lakini leo hii Chief wametuonyesha ubovu wa mpira wetu. Kiurahisi kabisa wamemuacha na hawajamuacha kimizengwe. Ni kama Morrison tu.
Unadhani kuna timu ya Tanzania inaweza kumuacha mchezaji kama Kotei au Morrison? Timu hiyo haiko. Narudia tena timu hiyo haipo. Naomba nirudie. Timu hiyo haipo. Zaidi kila timu inatamani kuwa nao vikosini mwao.
Simba ilipokuwa inafungwa zile 5-0, 5-0 msimu uliopita haikuwa inafungwa kwa bahati mbaya. Ilistahili. Timu yao ilijaza kundi kubwa la wachezaji wa daraja la wastani, unapokuwa na wachezaji wa daraja la wastani kisha ukacheza na timu za daraja la Al Ahly unategemea nini?
Chief waliomuacha Kotei ni moja ya timu ya kawaida kwa sasa. Hawajashinda ubingwa wa ligi kwa miaka mingi. Ni kama Pirates tu. Hawana ubavu wa kusogelea michuano mikubwa ya nje na ndani, ungetarajia timu ya namna hii iwe na kina Kotei, Morrison wengi ili kujijenga na kurudisha makali yao, licha ya udhaifu wao huo, lakini wamewatazama Kotei, Morrison wamewaona hawana wanachoweza kuwapa. Wameachana nao.
Ili timu zetu ili ziwe na uwezo wa kukaribia kushinda taji la Afrika zinatakiwa kusajili wachezaji mahiri kuwazidi Morrison na Kotei. Lakini hawa kina Kotei na Deo Kanda ni walewale.
Lakini kama timu zetu zitaendelea kuwakimbilia wachezaji walioachwa Chief, Pirates, Mazembe tujue wazi tuna safari ndefu kufika ziliko TP Mazembe, Al Ahly na wababe wengine.