- Safari ya Yanga, Mikononi mwa Dube
- Simba na Yanga nani anaongoza kuweka mpira kwapani.
- Yanga Waweweseka! Gamondi Nje!
- Fadlu Tunaamini anawapa Ubingwa Wekundu
- Manuel Neuer ana umri sawa na uchambuzi wa soka kwa kompyuta
PAPY Tshishimbi, Feisal Salum walikuwa na viwango vya kuridhisha msimu uliopita na viungo hawa wa kati waliweza kuisaidia Yanga SC kumaliza katika nafasi ya pili katika ligi kuu Tanzania Bara msimu uliopita- nafasi ambayo kimsingi inawapa nafasi ya kucheza michuano ya ligi ya mabingwa Afrika msimu ujao .
Baada ya Tanzania Bara kupata ongezeko la timu katika michuano ya Caf ( kutoka timu mbili hadi nne ) katika michuano yote- timu mbili katika ligi ya mabingwa na nyingine mbili katika Kombe la Shirikisho, kocha Mcongoman, Mwinyi Zahera anaendelea kukisuka kikosi chake kuelekea msimu mpya ambao Yanga wataanzia hatua ya awali mwezi ujao wa Julai.
KUIMARISHA NGOME…..
Moja kati ya matatizo ya haraka yaliyoigharimu Yanga msimu uliopita ukiachana na yale ya nje ya uwanja kama madai ya mishahara- ndani ya uwanja Yanga ilikabiliwa na matatizo ya kushindwa kuwa na wachezaji bora katika nafasi muhimu- golikipa, beki ya kati, kiungo mchezesha timu na eneo la wafungaji.
Katika ngome, Zahera alionekana kushindwa kupata mbadala wa aliyekuwa nahodha wa kikosi chake Kelvin Yondan hasa pale alipokosekana kwa sababu za kinidhamu ama za kimaslai binafsi. Abdallah Haji ‘Ninja’ alikuwa na msimu bora yeye binafsi, lakini bado hakuweza kuziba baadhi ya nyufa zilizoachwa na Mtogo, Vicent Bossou na ‘nahodha mstaafu’ Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Ninja alishindwa kujiongoza na kujipanga vizuri- rejea pambano ambalo Yanga walipopoteza 1-0 katika ‘Dar es Salaam-Pacha’ dhidi ya mahasimu wao Simba SC mwezi April mwaka huu. Vicent Andrew ‘Dante’ bado ameshindwa kujidhirisha kama mmoja wa mabeki bora wa kati nchini licha ya kuichezea Yanga kwa misimu mitatu iliyopita.
Dante amekuwa akicheza kwa kujituma, lakini kukosa kwake utulivu wakati anapokuwa na mpira kumeifanya Yanga kuwa matatizoni mara kadhaa msimu uliopita. Angalau beki ya Yanga ilikuwa na utulivu kiasi alipokuwepo Kelvin lakini kila walipocheza Dante na Ninja mambo yalikuwa mabaya hivyo njia mojawapo ya kuongeza ufanisi katika ngome yake Zahera akaona ni bora amsaini Mghana, Lamine Moro.
Yanga ilikuwa na matatizo makubwa katika ngome, eneo la golikipa lilikuwa ni sehemu iliyokuwa ikitia presha kubwa. Kuwasaini, Metacha Mnata aliyekuwa na msimu mzuri Mbao FC, Mkenya Farouk Shikalo ‘Mr. Cleenshets’ kutarejesha ubora na umakini uliokosekana wakati lango hilo lilipokuwa likilindwa na Mcongo, Klaus Kindoki na chipukizi Ramadhani Kabwili.
Kumekuwa na taarifa za mlinzi wa kushoto, Gadiel Michael kutakiwa na mahasimu wao Simba. Gadiel anaelekea kumaliza mkataba wake Yanga na ni mmoja wa wachezaji muhimu wa Yanga kwa misimu miwili iliyopita. Ally Sonso anaweza kucheza eneo hili la pembeni lakini huyu ni mlinzi bora wa kati na anaweza kutengeneza ukuta mzuri sambamba na Kelvin na Moro.
Kuondoka kwake ( Gadiel) hakurajiwi, lakini tayari Zahera aliona umuhimu wa kuongeza mchezaji bora Zaidi katika beki tatu baada ya kiwango cha wasiwasi kutoka kwa msaidizi wa Gadiel , Mwinyi Haji ambaye pia anamaliza mkataba wake hivi karibuni. Kumsaini Mrundi, Patrick Sibomana ni sehemu ya kuimarisha beki ya kushoto.
Ongezeko la Metacha, Shikalo, Moro na Patrick kutaimarisha ngome kwasababu usajili wao umezingatia mapungufu yaliyojitokeza kwa msimu mzima uliopita, labda Yanga watahitaji saini za walinzi wengine wawili wa pembeni na katika hili wanaweza kuwatazama, William Lucian ‘Galass’ kama msaidizi wa beki ya kulia na Paul Ngalema katika beki ya kushoto kama Gadiel ataondoka.
UNAMTAKA KAMUSOKO?
Abdulaziz Makame, Mnyarwanda, Issa Bigirimana, Mrundi, Mustafa Suleiman hawa wataongeza nguvu katika eneo la kiungo ambalo ni uhakika nyota kama Mcongo, Tshishimbi, Feisal, Rafael Daud watabaki kikosini msimu ujao.
Baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika timu yake ya Taifa ya Zimbabwe katika michuano iliyomalizika wiki iliyopita ya Cosafa Cup na michezo ya maandalizi kuelekea michuano ya Mataifa ya Afrika, Thaban Kamusoko amekuwa akipigiwa ‘chapuo’ aongezewe mkataba klabuni Yanga baada ya ule wa awali kuelekea mwisho. Kamusoko ni mchezaji kipenzi cha Yanga tangu alipojiunga na klabu hiyo katikati yam waka 2015 akitokea FC Platnum ya kwao Zimbabwe.
Alikuwa na misimu miwili bora mwanzoni lakini misimu hii miwili ya mwisho amekuwa akisumbuliwa mno na majeraha kiasi ambacho kimelekea kuporomoka kwa kiwango chake n ahata pale anaporejea ufanisi wake ni wazi si ule wa misimu ya 2015/16 na 2016/17. Ni mchezaji mzuri lakini umefika wakati wa klabu kukubali kuleta wachezaji wapya na hicho ndicho kilichofanywa na kocha Zahera.
Yanga inaweza kufanya vizuri bila Kamusoko na nyota huyo wa Zimbabwe ni kama anahitaji kukutana na changamoto nyingine mpya nje ya klabu yake ya sasa. Kusaini viungo hao watatu ni ongezeko zuri hasa kama wachezaji hao watafikia malengo yanayokusudiwa. Sioni nafasi ya Kamusoko katika mtazamo mpya wa klabu , ila katu siwezi kupinga ubora alionao.
NGUVU ZAIDI KATIKA MASHAMBULIZI…..
Mcongo, Heritier Makambo alifunga magoli 17 katika ligi kuu msimu uliopita- ukiwa ni msimu wake wa kwanza kucheza Tanzania. Makambo ameuzwa kwenda klabu ya Horoya AC ya Guinea, na huku aliyekuwa kinara wa pasi za mwisho Ibrahim Ajib akiondoka pia klabuni hapo, kocha Zahera amesaini washambuliaji watatu wa kigeni.
Mnamibia, Sadney Urikhob, Mzambia Maybin Kalego na Mganda, Juma Balinya wanaweza kuongeza nguvu ya kutosha katika ufungaji huku mchezaji pekee anayetaraji kuendelea kubaki kikosini humo Mrisho Ngassa akiungana nao.
Kama Mrundi, Amis Tambwe, Matteo Antony wataachwa waondoke nadhani Yanga wanapaswa kusaini angalau winga wawili na labda wanapaswa kumrejesha kikosini kijana wao mwenye kipaji kikubwa Yusuph Mhilu na kumpandisha Mustapha kutoka timu ya vijana.
Kiujumla hadi sasa Yanga imesaini vizuri wachezaji wapya na kikosi hicho kinaonekana kinaweza kurejesha ubingwa waliopoteza kwa misimu miwili mfululizo kwa mahasimu wao Simba. Zahera amesaini haraka timu yake na sasa akijiandaa kuiongoza timu yake ya Taifa katika michuano ya Mataifa ya Afrika huko Misri ni wazi hatakuwa na wasiwasi kuhusu msimu wake wa pili Yanga kwa sababu amesaini ‘kitaalam mno’