Mara baada ya Shirikisho la Soka nchini kutangaza ‘uzi’ (jezi) mpya kwaajili ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika itakayoanza tarehe 21 nchini Misri, wadau wengi wametolea maoni kuhusu jezi hizo. Mashabiki hao wanaona kama jezi haina ubora wa kutumika katika michuano hii, wengine wanaona kama ubunifu wake hauvutii na wengine kuhoji kuhusu rangi ya jezi husika hasa ya ugenini.
“Jezi hii imebuniwa kwa kuzingatia rangi ya bendera ya taifa (Tanzania)” Wallace Karia, Rais wa shirikisho la Soka nchini aliwaambia wageni na waandishi wa habari wakati akiongelea katika uzinduzi huu. Bendera ya taifa ina rangi nne, Kijani, Njano, Nyeusi na Blue, jezi hizi zimebeba rangi zote ingawa jezi ya ugenini tu ambayo ndio ina maswali mengi, ambayo imetumia rangi ya njano.
Kiujumla jezi ni nzuri na jezi ni sare ya kutambulisha timu, kwa hili tunaweza wapongeza TFF. Lakini, yawezekana wadau wengi wanatoa maoni yao sababu kwanza walitegemea mtengenezaji tofauti na pili kila mmoja anamatamanio yake kuhusu nini anapenda kuvaa.
“Nunueni Jezi hizi kama utambulisho wa taifa letu, na kwakuwa hatuna vazi la taifa, hii kwa sasa itatutambulisha” sehemu ya nukuu katika hotuba ya mgeni rasmi na mwenyekiti wa hamasa wa timu ya Taifa Stars, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Mh Paul Makonda. Jezi ni utambulisho, ni vazi, mvaaji wake anatakiwa kulitetea vazi hilo kwa tabia yake, muonekano na matokeo yake uwanjani.
Wachezaji wa Timu ya Taifa walio Misri ndio wamebeba mzigo huu mzito wa kuipa thamani jezi hii, matokeo yao uwanjani ndiyo yatafanya hii jezi kuwa bora au ovyo, kuwa ya ubunifu au la, kuwa ya bei rahisi au ghali, kuvalika hadi kanisani na misikitini au popote, kukaa nayo baa unakunywa au kwenda kutolea posa wakati wa kuoa.
Wachezaji wataonekana nadhifu katika jezi hii licha ya rangi, mashabiki wanaweza gawanyika kutokana na itikadi zao za utani wa jadi lakini hao hao nyumbani kwao wamehifadhi jezi za kina Romario, Ronaldo Di Lima na hata za kina Eto’o. Ndio mana tunasema, matokeo uwanjani ndio muhimu.
Mbwana Ally Samatta, baada ya miaka 39, ipe heshima jezi hii yenye rangi inayotambulisha utaifa wetu pamoja na yule twiga ambaye ni nyara za serikali, mnyama mwenye maringo…wacha turinge Afrika nzima. Hili kombe tufanye vizuri, ili kumbukumbu ziwekwe mlima Kilimanjaro na tuangaze Afrika nzima kama ilivyo mwenge wa uhuru.