- Safari ya Yanga, Mikononi mwa Dube
- Simba na Yanga nani anaongoza kuweka mpira kwapani.
- Yanga Waweweseka! Gamondi Nje!
- Fadlu Tunaamini anawapa Ubingwa Wekundu
- Manuel Neuer ana umri sawa na uchambuzi wa soka kwa kompyuta
Licha ya kufunga magoli saba na kutoa ‘usaidizi’ wa magoli yasiyopungua 15 katika ligi kuu Tanzania Bara msimu huu, Ibrahim Ajib bado hajadhihirisha ubora wa juu ambao Simba SC ina uhitaji kama timu yenye malengo makubwa Afrika.
Baada ya kufika robo fainali katika michuano ya ligi ya mabingwa Afrika msimu huu :wakiwa na nafasi kubwa ya kutetea ubingwa wa ligi kuu Bara, Simba imekusudia kuboresha kikosi chao kwa lengo la kufanya vizuri zaidi msimu ujao katika michuano ya ndani na ile ya Afrika.
Hakuna mwenye shaka kuhusu kipaji cha Ajib, lakini kwa mtazamo wangu Simba tayari imepiga hatua kubwa kiubora wakati ndani ya msimu miwili iliyopita ya kiungo huyo mshambulizi wa Yanga tumeshuhudia ‘kudumaa’ kwa ubora wake binafsi.
Inawezekana, Ajib ni kipenzi cha baadhi ya mashabiki, wanachama na viongozi wa Simba hali inayopelekea kusainiwa kwake, lakini kwa mtazamo ule wa mwekezaji mkuu, Mohamed Dewji kumsaini Ajib ni sawa na kuidumaza klabu.
Miezi miwili iliyopita, Dewji alisema hadharani kuwa timu yao ‘ina wachezaji wanne tu’ wenye hadhi ya juu, na kabla ya mchezo wa kwanza wa robo fainali dhidi ya TP Mazembe mwezi uliopita MO alisisitiza Simba itaingia katika soka la usajili barani Afrika na itajaribu kupambana na klabu kubwa za Afrika kuwania wachezaji.
Je , wachezaji wenyewe ndio hawa ‘taipu’ ya Ajib? Mchezaji mjivuni, mvivu na asiye tayari kupigania timu yake?
Kutoa zaidi ya Tsh. 80 milioni kwa mchezaji kama Ajib sawa, lakini je, mchezaji huyo ataongeza ubora gani mpya katika safu ya washambuliaji kama John Bocco, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi.?
Kwa aina ya uchezaji wa Ajib, tena akiwa nahodha wa klabu kubwa kama Yanga ni ‘aibu’ kuona akifanyiwa mabadiliko katika kila mchezo anaoanza.
Kitendo cha kocha Zahera Mwinyi kumuanzisha nje, na kumfanyia mabadiliko kila mchezo anaoanza ni wazi mchezaji huyo hana mazoezi ya kutosha na jambo hilo linachangiwa na uvivu wake ambao si mgeni kwa watu wa Simba.
Ili kupiga hatua mbele zaidi Simba inatakiwa kutuliza akili zao na kutazama kwanza ni wachezaji gani wana uwezo wa kuwaondoa kikosi cha kwanza Kagere, nahodha Bocco na Okwi, lakini kama wanafikiria kusaini wasaidizi tu wa washambuliaji hao watatu kamwe hawataweza kuzifikia timu kubwa za Afrika kama wanavyotamani.
Matamanio yao ni lazima yaendane na malengo. Kuboresha kikosi si tendo la kusaini wachezaji wapya tu, bali ni kusaini wachezaji bora zaidi ya waliopo sasa kikosini.
Ni afadhali kuendelea kusubiri ubora wa Mohamed Ibrahim, Adam Salamba kuliko kusaini mchezaji mvivu kama Ajib.
Ni nyongeza gani ya ubora ambao Ajib ataongeza katika timu ya Simba? Naamini ataenda kuwadumaza kina Kagere kwa maana hawatapata ushindani mpya kikosini jambo ambalo halitawasaidia wala kuisaidia klabu kukua kimchezo.