- Safari ya Yanga, Mikononi mwa Dube
- Simba na Yanga nani anaongoza kuweka mpira kwapani.
- Yanga Waweweseka! Gamondi Nje!
- Fadlu Tunaamini anawapa Ubingwa Wekundu
- Manuel Neuer ana umri sawa na uchambuzi wa soka kwa kompyuta
MKEYENGE sijawa Mwandishi mkubwa kiasi hicho cha kutisha watu. Sijawa wa hivyo. Ni Mwandishi mchanga ninayependa kujifunza na kumsikiliza kila mtu. Safari bado ni ndefu sana. Nilikotoka ni karibu, lakini ninakokwenda ni mbali. Mbali mno.
Katika majukwaa ya kimichezo yaliyonifunza mengi na kunifanya nitazamike japo kwa udogo wangu ni hili Kandanda ninaloamua kuliandikia kitu siku ya leo. Jukwaa hili huru naliheshimu sana.
Leo Kandanda limetimiza miaka nane tangu lilivyoanza kujihusisha na shughuli za kutoa taarifa za kimichezo. Kwangu hii ni miaka mingi. Nina miaka mitano ya uandishi, hivyo miaka minane kwangu lazima iwe miaka mingi.
……makala inaendelea baada ya tangazo…..
Kandanda imenilea, imenifunza, mwisho kabisa imenifungulia dunia kuwa ninachokitaka. Leo Mkeyenge sitazamwi tena katika jicho lile ambalo niliwahi kutazamwa huko nyuma. Kupitia jukwaa la Kandanda siku hizi natazamwa kwa jicho tofauti.
Siku hizi siandikii tena jukwaa hili. Lakini nimekuwa mdau mzuri na rafiki wa karibu kwa timu nzima ya Kandanda. Nimekuwa sehemu ya familia.
Ukimya wangu leo usingekuwa na maana bila ya kuandika chochote kile kinachoihusu Kandanda. Kuna sehemu ya moyo wangu ingenisuta kama ningekaa kimya katika muda ambao nilipaswa kuandika kitu.
Dizo Moja, Mkubwa Kambi, Saleh Geva, Patrick Dumulinyi, Nassor Binslum ni sehemu ya watu niliofahamiana nao Kandanda. Lakini leo wamegeuka kuwa rafiki zangu wazuri tunaoshirikiana mambo mbalimbali.
Hawa pamoja na rafiki zetu wengine tumejenga urafiki mzuri. Nisingefanya vyema kama siku hii ingenipita wima kama basi lililojaa kituoni bila kuandika chochote kile kinachoihusu jukwaa letu.
Jukwaa hili siku hizi lina vijana wengine wapya wanaozidi kuipeperusha bendera. Lakini uwepo wao hautufanyi kina Mkeyenge na Dizo tukiwa na maandiko yetu tushindwe kuyaandika. Hili ni kimbilio. Muda wote tunapokewa kufanya kazi.
Kuna muda unaweza kuona kama Kandanda haiko tena. Lakini ni tofauti. Patoo anafanya kazi kubwa kuipigania Kandanda iendelee kuwepo. Anatumia kila nguvu aliyonayo ili Kandanda isimame. Mashallah Kandanda imesimama imara.
Leo hii tuliyoshinda majumbani kwetu bila ya kwenda makazini kuadhimisha Sikukuu ya Mei Mosi, tuiingie katika tovuti hii kuona taarifa mbalimbali za kimichezo na makala za kutosha.