Sambaza....

Kocha mkuu wa timu ya soka ya Real Madrid Zinedine Zidane amewashukia wachezaji wake na kuwalaumu kwa kichapo walichokipata usiku wa kuamkia leo dhidi ya Rayo Vallecano kwenye muendelezo wa ligi kuu nchini Uhispani ‘La Liga’.

Madrid ilikumbana na kichapo cha 10 msimu huu kwa bao pekee la Adi Embarba katika kipindi cha kwanza na matokeo hayo yamemkera sana Zinadane na kuwatupia lawama wachezaji wake kuwa ndio sababu.

“Hatujafanya chochote leo, kuanzia dakika ya kwanza mpaka ya mwisho, kuna wakati unachezaji vizuri na unashindwa kufunga lakini leo tumeshindwa kabisa hata kutengeneza nafasi za kufunga, hatujafanya chochote kile vizuri, lazima tuwa na hasira kutokana na kiwango chetu, na mimi nina hasira kwa sababu tumetoa picha mbovu,” Zidane aliwaambia waandishi wa habari.

Hicho ni kichapo cha kwanza kwa Real Madrid kukipata kutoka kwa timu ndogo ya Rayo toka mwaka 1997, na hii ni mara ya kwanza baada ya zaidi ya miaka kumi kwa Real Madrid kupoteza michezo 10 kwenye msimu mmoja wa ligi.

Mpaka sasa Zidane ameiongoza Madrid michezo nane ya ligi toka aliporejea kwenye klabu hiyo mwezi Machi baada ya makocha wawili kutimuliwa (Julen Lopetegui na Santiago Solari) baada ya yeye kujiuzulu mwishoni mwa msimu uliopita kwa mafanikio makubwa ikiwemo kunyakuwa mara tatu taji la Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.

Sambaza....