Nilikuwa namsikiliza mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam , Paul Makonda akitoa maoni yake baada ya Serengeti Boys kufanya vibaya kwenye michuano ya Afcon.
Sina tatizo la maoni yake, maoni yake ni mazuri sana na tushawahi kuwa na aina hiyo ya maoni kutoka kwa watu wengi sana hapa nchini lakini tatizo huishia midomoni mwa wengi.
Hakuna kinachofanyika baada ya kuongelewa kwa maoni chanya kama hayo. Yani huu utamaduni tumejijengea na hatuna hofu nao kabisa.
Tunaongea, tunafurahisha masikio ya Watanzania wengi na baada ya hapo linapita, na wakati mwingine tunasahau kabisa kuhusiana na matatizo yetu ya msingi.
Huwa tunakuja kukumbuka matatizo yetu ya msingi kipindi ambacho tumepigwa tena kipigo kingine na timu yoyote kutoka nje.
Hadithi hubaki ile ile , MFUMO. Hii ndiyo hadithi ambayo huongelewa kila siku. Inaongelewa sana, tena sana na kuna kipindi huwa naona inachosha.
Mpaka muda huu mimi binafsi imeshanichosha hii hadithi ya MFUMO. Haijaanza kuongelewa Leo, au haijaanza kuongelewa na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam.
Imeongelewa tangu zamani na watu wengi sana lakini hakuna kitu cha muhimu ambacho ni chanya ambacho kishafanyika kwa vitendo kuhusiana na neno MFUMO.
Kuna wakati niliandika kitu kimoja kuhusiana na hizi kamati ambazo huundwa kwa matukio maalumu. Yani tukiona timu za Taifa zinahitaji ushindi Fulani tunaiunda haraka haraka hiyo kamati.
Zimekuwa nyingi sana, na zina lengo lile lile tu ambalo huonekana kama ni lengo mama, yani KUZISAIDIA TIMU ZA TAIFA ZISHINDE. Iwe kwa kuhamasisha mashabiki kuingia kwa wingi uwanjani au kutafuta pesa za hamasa kwa ajili ya timu.
Yani huwa tunajaribu kutafuta furaha ya muda tu kila wakati na inapotokea tumefungwa tunarudi kwenye ile hadithi yetu pendwa MFUMO.
Hapa ndipo huwa nashangaa kitu kimoja. Unaweza kukuta mwanakamati wa hizi kamati mwanzoni mwa Kazi za hizi kamati anajitolea kweli, lakini mwishoni baada ya kufungwa hujitoa kwa kujitetea kwa kutumia kivuli cha MFUMO.
Hapa ndipo ninapojiulizaga kumbe huwa tunajua tatizo letu tangu awali tunapochaguliwa kwenye hizi kamati, lakini hatujawahi kuona kuwa hizi kamati siyo suluhusiho.
Hizi kamati haziwezi kutupa furaha ya muda mrefu. Hili huwa tunaliona kabisa lakini huwa tunaogopa kulisema awali na kulisema mwishoni baada ya mambo kuonekana yameenda katika mstari mbaya.
Na kuna wakati hata viongozi wetu wa shirikisho la mpira wa miguu hawafikirii kabisa kuhusiana na miaka 10 ijayo, wanafikiria kuhusiana na siku waliyopo tu.
Ndiyo maana huhusika kuunda kamati za matukio tu. Hatujawahi kuona kamati inaundwa kwa ajili ya kutafuta dawa sahihi ya ugonjwa.
Na kibaya zaidi hata watu ambao huwa wanafuatwa na viongozi wetu wa shirikisho la mpira wa miguu huwa wanatumika vibaya, hawatumiki kwa manufaa ya Taifa letu.
Mfano mzuri ni kwa mzee wetu Reginald Mengi. Huyu alifuatwa aje kuwa mlezi wa Serengeti boys hii ambayo imefanya vibaya katika michuano hii Afcon ya vijana walio chini ya umri wa miaka 17.
Haya ni matumizi mabaya kabisa ya rasilimali watu. Tena matumizi ya HOVYOO KABISA!. Matumizi yasiyokuwa na tija kwa Taifa letu ndiyo maana mwisho wa siku mzee wa watu kaishia kutoa ahadi za milioni 20 na gari.
Huyu mzee ni mwenyekiti wa sekta binafsi hapa Tanzania. Chama cha sekta binafsi hapa Tanzania kinaongozwa na huyu mzee.
Yani Wafanyabiashara wakubwa wote hapa nchini Tanzania wanamsikiliza Reginald Mengi akiwa mbele yao kwenye meza kubwa ya vikao vyote.
Huyu ni mfanyabiashara tajiri mkubwa barani Afrika ambaye kwenye orodha ya Forbes huyu yuko kwenye 20 bora ya matajiri wakubwa Afrika.
Unaona namna ambavyo TFF walivyo na bahati ya kukutana na watu ambao wanauwezo wa kubadilisha sura ya mpira wa nchi yetu lakini wanawatumia vibaya?
Huyu Reginald Mengi hakupaswa kabisa kuwa mlezi wa Serengeti Boys. Huyu angepewa jukumu moja tu ambalo lingeenda kama ombi kubwa kwake.
Huyu ni mwenyekiti wa sekta binafsi hapa Tanzania, sekta binafsi zimebeba matajiri wakubwa sana hapa nchini.
Wangemuomba kwa nafasi yake, kwa ushawishi wake mkubwa ambao anao angeongea na wafanyabiashara wenzake wafanye kitu kimoja kwa pamoja.
Kitu chenyewe ni kujenga kituo cha kuibua, kulea na kukuza vipaji vya soka hapa nchini. Maombi ya TFF yangeweza kuambatana kwa njia mbili.
Njia ya kwanza ni kwa Wafanyabiashara hao wakiongozwa na Reginald Mengi kukusanya nguvu zao kwa pamoja na kufanya harambee ambayo ingekuwa mahususi kwa ajili ya kujenga kituo hiki na kukibadhi kuwa Mali ya TFF.
Au wangeongea nao kibiashara, kuwa Wafanyabiashara hawa wangeamua kujenga kituo hiki wakiendeshe kibiashara kwa faida yao wenyewe.
Yani wakimiliki wao kwa share ndani yao. Na kiwe Mali yao, yani vijana ambao watauzwa kupitia hiki kituo faida ingebaki kuwa kwao.
Hii iwe njia moja wapo ya wao pia kuhusika katika uwekezaji wenye faida kwa sababu mpira wa miguu ni sehemu inayoingiza pesa nyingi sana.
Kwa hiyo kwa kituo hiki kingezalisha wachezaji ambao wangekuwa na msaada mkubwa sana kupata timu imara ya vijana pamoja na ile timu kubwa ya Taifa.