Sambaza....

Klabu ya Simba tayari imeshafuzu hatua ya robo fainali baada ya kuichapa AS Club Vita ya Congo kwa goli 2-1. Ushindi huo unawafanya wafikishe jumla ya alama 9 katika nafasi ya pili nyuma ya vinara Al Ahly ya Misri yenye alama 10 na inayoongoza kundi D.

Hatua ya makundi ilijumuisha jumla ya makundi manne, yaani kundi A, B, C, na D. katika kundi A, Wydad Casablanca na Mamelodi Sundowns zimeshafuzu, Kundi B,ni Esperance de Tunis na Horoya zimeshafuzu, Kundi C, TP Mazembe na CS Constantine zimeshafuzu pia na kundi D Al-Ahly na Simba zimeungana na nyingine kufuzu hatua ya robo fainali.

Kwa mujibu wa sheria za CAF katika mashindano ya Klabu bingwa, vinara katika makundi watacheza na wanaoshika nafasi za pili. Na timu za kundi moja haziwezi kukutana.

Hii ina maana kuwa Simba SC lazima ikutane na kati ya timu hizi tatu, WYDAD CASABLANCA ya Morocco , ESPERANCE DE TUNIS ya Tunisia au TP MAZEMBE ya Congo DRC.


Droo itakayochezeshwa machi 20 siku ya Jumatano mwaka huu, ndio itakayokuwa mwamuzi halisi juu ya timu gani inatakiwa kucheza na Simba, huku timu zilizoongoza kundi hupewa haki ya kupata uenyeji katika mechi ya marudiano. Hii inamaanisha kuwa, Simba ni lazima itaanzia nyumbani kwa kuwa imemaliza katika nafasi ya pili katika kundi D.

Hatua hii ni hatua ya mtoano, idadi ya magoli kwa mechi ya nyumbani na ugenini, kama yatakuwa yapo sare, hakuna dakika za nyongeza, kinachofuata ni mikwaju ya penati.

Katika droo hiyo, kutakuwa na makundi manne, yenye timu mbili mbili, mshindi wa kundi la kwanza atacheza na mshindi wa kundi la pili , na mshindi wa kundi la tatu atacheza na mshindi wa kundi la nne, kupata timu mbili za kwenda kukwaana katika mchezo wa fainali.

Mechi za mzuunguko wa kwanza zinatarajiwa kupigwa kati ya tarehe 6-7 ya mwezi Aprili na zile za raundi ya pili ni kati ya tarehe 12-13 ya mwezi huo huo.

Sambaza....