Goli 2-0, tena unafungwa nyumbani kwako ? na unafungwa na timu ambayo imesheheni nyota wengi barani ulaya.
Na kibaya zaidi unatakiwa kukutana nao katika uwanja wao wa nyumbani wakiwa na faida ya magoli 2-0 waliyoyapata katika uwanja wa ugenini.
Na ni mechi ya mtoano ambayo unatakiwa kupindua matokeo ili umtoe. Na mtu wa kumtoa ni PSG yenye nyota wengi tena nyumbani kwake.
Na kibaya zaidi Ole Gunnar akasafiri mpaka Paris akiwa na rundo kubwa la wachezaji ambao walikuwa wodini. Wachezaji 11 hawakuwepo katika safari hii.
Na unatakiwa kupindua matokeo ugenini na huna wachezaji muhimu katika kikosi chako. Na mashabiki wanakutazama kama mwokozi wao.
Huu ulikuwa mlima mrefu na mgumu sana kuupanda. Wengi walikuwa hawana uhakika kama Manchester United wanaweza kupindua matokeo ya mechi hii.
Hata kabla ya mechi hii kocha wa muda wa Manchester United alipoulizwa kuhusu kupindua matokeo haya dhidi ya PSG cha kwanza alitoa tabasamu.
Tabasamu ambalo lilisindikizwa na maneno ya kutia moyo, maneno ya kishujaa, maneno ya mwanajeshi ambaye alikuwa tayari kufa kwa ajili ya nchi yake.
Maneno ambayo ni tiba tosha kwa mtu ambaye anaonekana kukata tamaa kutokana na ugumu anaopitia kwa wakati huo.
Ole Gunnar , alisema kuwa “milima ipo kwa ajili ya kupandwa”. Hiki ndicho alichokiongea Ole Gunnar baada ya kuulizwa kuhusiana na kupindua matokeo.
Ugumu tumeumbiwa sisi wanadamu. Huwezi kukwepa ugumu hata siku moja kwenye maisha ya mwanadamu.
Huwezi kusema unaishi kwenye maisha wakati unakimbia ugumu unaokukabili. Ndicho kitu ambacho Ole Gunnar alichomaanisha.
Hakutaka kabisa kuamini katika kukimbia tatizo aliamini kabisa kwenye kukabiliana na tatizo. Hakuamini kwenye kushindwa kujaribu kufanya kitu, ila aliamini kwenye kujaribu kufanya kitu hata kama angeshindwa kulifikia.
Hiki ndicho kilichokuwepo moyoni mwa Ole Gunnar, alikiongea huku akiwa anaamini kabisa hana wachezaji nyota kwa asilimia kubwa.
Aliongea akijua kabisa yuko nyuma kwa magoli 2-0 , lakini alikuwa anaziamini dakika 90 zilizokuwa mbele yake.
Aliamini zinaweza zikabadilisha ugumu kuwa urahisi . Na ndicho kitu kilichotokea kwa Manchester United.
Waliweza kupindua matokeo, hakuna jambo gumu kwenye mioyo yenye nia. Simba wanatakiwa kuvaa mioyo yenye nia.
Mioyo ya upiganaji, mioyo ya kianajeshi waliotayari kufia kwa ajili ya nchi yao. Simba wanatakiwa kuvaa mioyo ya ushindi.
Mioyo isiyokata tamaa hata kidogo. Hiki ndicho kinachotakiwa kuwepo ndani ya mioyo ya wachezaji wa Simba.
Najua kabisa As Vita ni timu ngumu sana hapa Afrika. Wana fainali wa kombe la shirikisho barani Afrika msimu uliopita.
Na michuano hii wamekuwa wakifanya vizuri sana kwa miaka ya hivi karibuni. Na tayari wana ile hali ya wao kufika mbali kwenye michuano ya CAF.
Hali ambayo itawafanya wao kwenye mechi hii kucheza kwa kuhakikisha wanapata matokeo ambayo yatawapa nafasi kubwa ya kufika robo fainali.
As Vita wanaitaka sana hii nafasi tena sana. Hawatokuja Tanzania kama watu ambao hawana chochote cha kutafuta.
Hii mechi ni fainali, na ugumu zaidi ni kuwa katika kundi hili mechi zote za mwisho za kundi hili ni fainali. Yani kila atakayeshinda kwenye mechi za mwisho za hili kundi ana nafasi kubwa sana ya kufika robo fainali ya michuano ya CAF.
Hapa ndipo ugumu unapokuja, na hapa ndipo Simba wanapotakiwa kabisa kuelewa kuwa ugumu katika maisha ya mwanadamu huja kwa sababu ya kumpa nafasi mtu kufanikiwa.
Hakuna ugumu unaokuja kwenye maisha ya mwanadamu kwa ajili ya kumbomoa. Kubomolewa huja pale mtu anapopokea huo ugumu.
Mapokeo ya ugumu ndiyo humwimarisha mtu. Ole Gunnar alipokea ugumu wa mechi ile dhidi ya PSG kama mtihani wanaotakiwa kufaulu.
Na walifanikiwa kufaulu, Leo hii Ole Gunnar anafikiria atapangwa na nani kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani ulaya.
Simba wanatakiwa kupokea ugumu huu kama mtihani ambao wanatakiwa kuufaulu kwa lazima. Ndiyo maana nawasisitiza kuwa milima ipo kwa ajili ya kupandwa.