Kwa mchina ndiyo jina ambalo lilikuwa limezoeleka sana , hili ndilo jina ambalo lilitumika kuiita uwanja wetu wa Taifa.
Wengi walizoea, jina liliwakaa sana wakawa wanaita tu bila hofu na ikafikia hatua kuwa ikawa kawaida kwa uwanja huo kuitwa KWA MCHINA.
Kwa kifupi lilikuwa kama jina rasmi la uwanja huo bora kabisa ambao tuliachiwa kama zawadi na Raisi wa awamu ya tatu , Ndg, Benjamini William Mkapa.
Juzi mheshimiwa Waziri Harrison Mwakyembe alitoa tamko la kiserikali kuwa ni marufuku kwa mtu yoyote kuita uwanja huu wa Taifa kuwa KWA MCHINA.
Tamko hili mimi naliunga mkono sana, na nina mpongeza sana waziri Harrison Mwakyembe kwa tamko hili.
Lakini kuna kitu kimoja kinabaki ambacho naamini bado hakijafikiwa muafaka sahihi wa jina gani sahihi ambalo linastahili kutumika kwenye huu uwanja.
Sawa!, nimekuwa nikisikia kuwa uwanja huu ukiitwa KWA MKAPA tangu Waziri Harrison Mwakyembe atoe tamko la kusitisha matumizi ya jina la KWA MCHINA kwenye uwanja huu.
Mimi naamini kitu kimoja, naamini katika mjadala mpana ili kufikia kitu bora chenye mafanikio ambayo ni chanya kwa maendeleo ya taifa letu.
Nina imani kabisa katazo la Waziri Harrison Mwakyembe la kusitisha matumizi ya jina la KWA MCHINA lilikuwa linatakiwa lije na mjadala wa kitaifa.
Mjadala wa jina gani ambalo ni sahihi kutumika kwenye uwanja huo ambao una sura kubwa ya kitaifa. Uwanja ambao kwa sasa ni bora sana kwa nchi yetu.
Tuanzie hapa kwa pamoja!, mimi naunga sana juhudi za Mheshimiwa Benjamin William Mkapa kwa kutuletea huu uwanja.
Lakini siungi mkono uwanja huu kuitwa jina lake. Kwa sababu tu za kibiashara. Tunamheshimu sana Mheshimiwa Benjamin William Mkapa.
Lakini kwa sasa tupo kwenye dunia ya kibiashara. Dunia ambayo wengi hutumia majukwaa mengi kutangaza bidhaa zao.
Nchi yetu ina bidhaa nyingi sana , na jukwaa la uwanja wa Taifa ni kubwa sana ambalo linaweza kutumika kwa maslahi mapana ya nchi yetu.
Twende taratibu tu!, uwanja wetu huu ndiyo uwanja ambao mechi nyingi za kimataifa huwa zinafanyika katika uwanja huu.
Timu nyingi kutoka mataifa mbalimbali huwa zinakuja kwenye uwanja huu kwa ajili tu ya kushiriki michuano mbalimbali ya kimataifa.
Hapa ndipo tunatakiwa kupafikiria vyema sana kwa ajili ya masilahi mapana ya taifa letu ( hasa hasa masilahi ya bidhaa zetu ).
Ngoja nikupe mfano mdogo, nchi yetu ina fahari nyingi sana ambazo kimsingi huwa hazitangazwi sana nje ya nchi yetu.
Ndiyo maana kuna watu kutoka nje huwa hawajui hata mlima Kilimanjaro uko Tanzania, kitu ambacho Wakenya hukichukua na kuanza kujitangaza kuwa wanamiliki mlima Kilimanjaro.
Hii ni kwa sababu moja tu , hatujachukua muda mwingi kwa ajili ya kutangaza fahari zetu nje ya nchi ili mataifa yajue bidhaa zipi tunazimiliki.
Tuna bidhaa mbalimbali ambazo ni bidhaa kubwa za kujivunia kama hifadhi kuu ya Serengeti, Mlima Kilimanjaro.
Tuna bonde la Ngorongoro , bonde la nne kwa ukubwa duniani. Tuna mlima mrefu barani Afrika, mlima Kilimanjaro.
Tuna madini ambayo yanapatikana Tanzania pekee, madini ya Tanzanite. Ni bidhaa kubwa tuliyonayo na ni fahari yetu.
Lakini pamoja na kuwa na bidhaa kama hizi ambazo ni bidhaa bora, nchi yetu imekosa sehemu ya kutangazia bidhaa zetu.
Ndiyo maana kuna baadhi ya nchi hutangaza baadhi ya bidhaa zetu kuwa ni zao. Na hii ni kwa sababu tu hatujatoa nafasi kubwa ya kuvitangaza vya kwetu.
Tuko kwenye dunia ambayo ni ya kibiashara , dunia ambayo unatakiwa utangaze bidhaa yako ili kukuza masoko na mauzo yako.
Moja ya sehemu nzuri ya kutangazia bidhaa ni kwenye michezo mbalimbali ikiwepo mpira wa miguu. Mchezo ambao hufuatiliwa kwa ukubwa sana.
Kwa sababu tu umeshika hisia za watu wengi. Ukitangaza bidhaa yako sehemu ambayo ina hisia za watu wengi basi ni nafasi kubwa ya kupata masoko mapya na kukuza mauzo.
Kama ambavyo nimesema huko juu, uwanja wetu wa Taifa huwa unapokea timu za kimataifa kwa ajili ya mechi za kimataifa.
Hapa kuna faida kwa sababu kuna wageni huwa wanakuja. Wageni hawa wakija lazima wapate hamu ya kujua vingi vya kwetu.
Kwa mfano, uwanja ukawa unaitwa Tanzanite Stadium , au Serengeti Stadium. Mgeni atataka kujua Vinci kuhusu Tanzanite, au Serengeti.
Pamoja na kwamba kuna wageni watakuja huku. Pia mchezo husika utatangazwa na vyombo vya kimataifa.
Vyombo ambavyo vitataja jina la uwanja. Jina ambalo litawafanya watu wajue mengi kuhusu jina husika na mwisho wa siku kutakuwa na faida kubwa kibiashara.
Mimi natamani tulitazame kwa jicho la kibiashara ya bidhaa zetu ambazo tumeshindwa kuzitangaza ili nchi yetu inufaike kibiashara.
Tumkumbuke Mheshimiwa Benjamin William Mkapa katika historia ya Tanzania ambayo inamtambua kama Raisi wa awamu ya tatu.
Tumkumbuke kupitia hospitali ya kimataifa ya Dodoma, tumkumbuke kupitia barabara na pia tumkumbuke kuwa ndiye aliyejenga huu uwanja lakini tuvae miwani ya kibiashara kwenye jina la uwanja huu.