“Thierry Henry ana sifa zote za kuwa kocha mzuri na mwenye mafanikio” ni kauli ya kocha Arsene Wenger aliyoitoa Jumapili alipoulizwa kama kutimuliwa kwa Henry katika klabu ya AS Monaco kunaweza kumuathiri na kuharibu maisha yake ya ukocha.
Wenger mwenye umri wa miaka 69 amesisitiza kuwa Henry bado ni kocha mzuri mwenye kila sifa na kwamba ilikuwa bahati mbaya tu kwake kuichukua Monaco ikiwa katika hali mbaya ya kupambana kutoshuka daraja.
“Katika kazi yetu, ni namna nyingine pale unapoanza msimu, kama mambo hayataenda sawa, unakuwa una miezi sita ya kurekebisha, kama utapewa kibarua Oktoba na timu ipo katika hali mbaya unakuwa na miezi mitatu pekee ya kutengeneza timu, kwa sababu mwezi Januari kila mtu anaanza kuchanganyikiwa na mambo yanaweza kuwa mabaya zaidi,”
“Hicho ndicho kilichomtokea Henry, ni kama kusema alikuwa na muda mchache wa kutengeneza timu, sasa kwa namna ambavyo ataweza kuondokana na umbwe la kufukuzwa na kurudi akiwa anajiamini zaidi hilo ndilo la muhimu, naamini anasifa na ari ya kupigania kazi yake na matokeo ya kazi bora hupimwa kwa muda mrefu kidogo” Wenger amesema.
Henry mwenye umri wa miaka 41 alifukuzwa na AS Monaco baada ya kuandikisha matokeo mabovu toka alipopewa timu mwezi Oktoba, akishinda michezo miwili pekee kati ya 15 ya ligi aliyoiongoza Monaco.
Thiery Henry alikuwepo kwenye kikosi cha kocha Wenger ambacho kilichukua ubingwa wa ligi ya England bila kupoteza mchezo wowote katika msimu wa mwaka 2003/2004.