Hii ndiyo sherehe rasmi ya mpira wa miguu. Sherehe ambayo kila mtu hutamani kuishuhudia kwa jicho lake na kuisikia kwa masikio yake.
Nchi nzima huwa inasimama kwa dakika 90 , presha hupanda kwa mashabiki wengi wa mpira wa miguu na hii ni kwa sababu moja tu. Timu hizi zimebeba mapenzi yetu ya soka, ndiyo timu ambazo zimeigawanya Tanzania katikati. Kuna pande mbili za Tanzania.
Upande wa kwanza ni ule ambao una rangi ya njano na kijani. Na upande mwingine ni ule ambao una rangi nyekundu na nyeupe.
Kwa kifupi kuna mikoa miwili pekee ya kimpira hapa Tanzania. Mkoa wa Jangwani na mkoa wa Msimbazi. Hawa ndiyo wazee wa mpira wetu.
Wamiliki halali wa mpira wetu na ndiyo watu wenye mafanikio makubwa sana kimpira hapa Tanzania. Ndiyo maana zimefanikiwa kuwa na mashabiki wengi nchini.
Ndiyo maana hata mechi hii huangaliwa sana. Ndiyo mechi ambayo kila jicho hutupia kwenye uwanja wa Taifa.Ndiyo mechi ambayo huwa inafanya shughuli nyingi za kitaifa kusimama mapema zaidi ili tu watu wawahi kuangalia hii mechi.
Ndiyo mechi ambayo huonekana ni sikukuu , tena sikukuu kubwa. Tena sikukuu yenye hisia kubwa sana ndani ya nchi hii.Hisia ambazo huanzia kwa mashabiki mpaka kwa wachezaji ndani ya uwanja. Hisia ambazo huleta presha kubwa sana kuanzia kwa mashabiki mpaka kwa wachezaji.
Ni kitu cha kawaida sana kwa mechi hii kumuona mchezaji ambaye huonekana ni bora kutokuonekana bora kwenye mchezo huu.Yani ni kitu cha kawaida sana. Kwa sababu tu mechi hii huwa na presha kubwa sana. Presha ambayo husababisha wachezaji wazuri kucheza chini ya kiwango.
Lakini kuna wakati kwenye hii mechi huwa iñaibua mashujaa ambao huwa hawatazamiki kuwa mashujaa. Lakini kwenye mechi hii huwa wanakuwa mashujaa.
Hapana shaka kwenye mechi iliyopita ya Simba na Yanga, shujaa aliyeibuka ni golikipa wa Yanga , Beno Kakolanya.Huyu ndiye aliibuka kuwa shujaa kwenye hii mechi. Aliikoa sana Yanga. Aliilinda sana Yanga na mikono yake ilikuwa shupavu kuhakikisha timu yake haipotezi.
Alifanikiwa sana kwenye hili. Mashabiki wengi wa Yanga walimpenda na walijivunia sana kuwa na golikipa kama Beno Kakolanya.Kwao wao Beno Kakolanya alionekana mtu muhimu zaidi kwa sababu tu aliwaokoa kwenye midomo ya Simba, Simba aliyekuwa na njaa Kali.
Leo hii tunapozungumza Beno Kakolanya hayupo tena na Yanga. Hana uhakika wa kucheza tena kwenye mechi ya leo.
Hii ni kutokana na kufarakana na kocha wake mkuu Mwinyi Zahera. Macho na masikio ya wana Yanga yapo kwa kinda Ramadhani Kabwili.
Golikipa wa zamani wa Serengeti Boys, Serengeti Boys iliyoshiriki michuano ya Afcon mwaka 2018 huko Gabon.
Huyu ana nafasi kubwa sana ya kuitetea Yanga kama ambavyo Beno Kakolanya alivyofanya katika mechi iliyopita iliyowakutanisha Simba na Yanga.Najua ni mchanga sana , hajakomaa sana kuhimili presha kubwa ya mechi kama hizi. Mechi hii ni kubwa sana kwake.
Kwa sababu tu hajawahi kusimama kwenye mechi kubwa kama hii, tena mechi yenye presha kubwa kama hii.Mechi iliyobeba hisia kubwa. Lakini kuna kitu kimoja ambacho anachotakiwa kukifirikia wakati anaenda kudaka kwenye hii mechi.
Anatakiwa kufikiria namna ambavyo anaweza kuwa shujaa ndani ya dakika 90. Ushujaa ambao utamfanya shabiki wa Yanga amsahau kabisa Beno Kakolanya.
Kipindi hiki mashabiki wa Yanga wamegawanyika mara mbili, wapo wanaomkumbuka Beno Kakolanya na wapo ambao hawataki kabisa kumkumbuka Beno Kakolanya.
Najua wanaweza wakawa pamoja baada ya mechi ya leo. Na wakufanya wawe pamoja ni Beno Kakolanya pekee. Huyu ndiye mwenye dhamana ya kuwafanya mashabiki wa Yanga kuwa pamoja.
Kiwango atakachokionesha ndicho ambacho kitawaleta mashabiki wa Yanga kuwa wamoja tena. Kama Ramadhani Kabwili ataonesha kiwango kibovu kwenye mechi kama ya leo basi mashabiki wengi wa Yanga watakuwa pamoja.
Wataungana kumkumbuka Beno Kakolanya. Lakini kama Ramadhani Kabwili atafanya vizuri kwenye hii mechi basi mashabiki wengi wa Yanga watakuwa pamoja kwa kutomkumbuka Beno Kakolanya.
Ramadhani Kabwili amebeba dhamana ya kuwakutanisha mashabiki wa Yanga na hii ni nafasi yake kubwa ya kuwa shujaa. Ushujaa ambao utamsaidia yeye kwenye maisha yake ya mpira wa miguu.