Nakumbuka kipindi nikiwa mtoto, nilikuwa sio mpenzi sana wa shule. Likizo na sikukuu kwangu zilikuwa ni sherehe nilizozisubiri kwa hamu kubwa. Nilikuwa nachukia sana kuona sikukuu ikiangukia siku za wikiendi maana ni sawa na bure.
Enzi hizo, wengine wanaziita zilipendwa, lakini hadi sasa hali bado kwa watoto wetu, nao hawana morali kubwa kiasi kwamba wakisikia shule imefungwa ghafla wanafurahi, hahahahaaha!, kicheko hiki hakina maana kuwa naifurahia hii hali bali napata fursa ya kukumbuka mbali.
Juzi tu kipindi Simba SC inafungwa na Bandari kutoka Kenya, katika mashindano ya SportPesa, niliona mambo mengi, ikiwemo mashabiki kumzonga kocha, Patrick Aussems, wengine wakitaka aondoka awaachie timu yao, wengine wakiuliza juu ya kocha msaidizi, kiufupi mashabiki walilalama.
Mwenyewe nashangaa! Tangu atimuliwe Masoud Djuma hakukuwa na kocha msaidizi ndani ya Simba, na siku zote hizo mashabiki hawakuwa wakilalamika, sababu Simba ilikuwa ikipata matokeo lakini mambo kwenda mrama kidogo, zogo linaanza, hii maana yake mashabiki wengi wanapenda timu ishinde tu.
Muendelezo wa nilichokiona nikakishuhudia tena katika mechi ya kutafuta mshindi wa tatu dhidi ya Mbao katika mshindano hayo hayo. Mashabiki wa Simba walikuwa wakihesabika uwanjani, walionekana kuisusa timu yao na hata wachache waliokuwepo waliishia kuwazomea wachezaji wa Simba mara wanapokuwa na mpira.
Hiki kinachotokea sasa Msimbazi naweza kukiita ni hasira, jazba na kuendeshwa na mapenzi kuliko soka katika uhalisia wake. Huwezi ukawazuia mashabiki kufanya wanachofanya kwa kuwa wao hawana mamlaka ya kiuongozi, sehemu pekee ya wao kutaka mabadiliko ni kuonyesha vitendo kama hivi, mashabiki wengi hupenda kila kitu kiwe vizuri kwa wakati wote, yaani timu ni lazima ipate matokeo kwa kila namna.
Tangu Simba ifungwe goli 5 dhidi ya AS Club Vita, morali ya timu imeshuka kwa kiasi kikubwa, wachezaji wanacheza lakini unawaona kabisa wanashindwa kujiamini. Hali hii ikitokea kwa timu yoyote, mashabiki ndio watatuzi wakuu, kwani wakiamua kuikubali timu yao licha ya matokeo mabovu, morali ya timu hupanda na kurudi kama zamani.
“kazi ya kocha na viongozi ni kutayarisha wachezaji kiakili, kwa sababu kile kidonda cha kufungwa 5 kipo, inafaa kidonda kile kipone kwenye vichwa vya wachezaji, ili kupona kunahitaji la kuwaingizia maneno mengi sana, huwezi kwenda kucheza na Al Ahly ukiwa na mbinu pekee, matokeo ya Congo yanaweza yakajirudia kama wachezaji hawata andaliwa kiakili” kocha wa Yanga SC, Mwinyi Zahera akiwazungumzia na kuwashauri Simba.
Kwa maneno hayo ya Zahera unaweza ukaona ni dhahiri kuwa, mashabiki na wachezaji wote wana matatizo ya kisaikolojia baada ya kipigo na muendezo wa matokea yasiyo ridhisha kwa timu.
Labda tu niseme kuwa, ni mapema sana kwa mashabiki na timu kwa ujumla kuumizwa na kushangazwa na matokeo kama haya, ni muda wa kuupenda mchezo wenyewe kabla ya kuleta maslahi ya Ushabiki na unazi.
Acha nikukumbushe juu ya ratiba ya Simba kwa mwezi februari, tarehe 2, watacheza na Al Ahly kule Misri na tayari Simba imeshasafiri, tarehe 6 Simba wataanza kula viporo, kwa kuwakaribisha Mwadui FC, tarehe 12 watawacheza na Al Ahly, hapa nyumbani, baada ya gemu hiyo tarehe 16 watakutana na Yanga, 19, watakuwa ugenini kwa A. Lyon, tarehe 22 dhidi ya Azam Fc na tarehe 26 watakuwa kule Iringa kucheza na Lipuli.
Umeiona hiyo ratiba, yaani Simba itakaa siku tatu hadi nne kabla ya kucheza mechi nyingine. Angalia huu mtiririko, Al Ahly,Mwadui, Ah Ahly, Yanga, A. Lyon, Azam na kisha watamaliza na Lipuli ugenini.
Ndani ya mwezi februari, Simba itacheza mechi 7, itakaa siku 3 na kucheza katika mechi za Yanga, A. Lyon na Azam ikiwa ni siku 4 pekee dhidi ya Al Ahly na Lipuli.
Kiufupi mwezi wa pili kwa Wekundu wa Msimbazi ni mchakamchaka, hakuna kulala wala mapumziko . hapa ndio ile dhana ya kikosi kipanda inatakiwa kuonekana katika mapana yake.
Haya! Kwa mfululizo wa mechi hizo zote, unaziweka wapi afya za mashabiki wa Simba ambao wanapaniki timu ikifungwa? Unataka kuniambia kuwa, Simba itawaridhisha mashabiki wake kwa kupata ushindi kwa kila mechi? sawa ! labda “YES WE CAN”.
Mashabiki ifike wakati wanatakiwa wajue kushinda au kushindwa ni aina za matokeo ambayo ni lazima wayakubali. Kwa kile kinachokuja, ni vema kwa mashabiki wa Simba kujiweka sawa kisaikolojia maana lolote linaweza kutokea.
Mwezi februari ni mwezi wa kujifunza uvumilivu, yaani kuepuka kubeba matokeo mfukoni kabla ya mechi kuchezwa. Katika mwezi huu wa pili Simba inatarajiwa kula viporo vyake vitatu, dhidi ya Mwadui, Azam na Lipuli na lolote linaweza likatokea, kwa jinsi ligi ilivyo ni sawa na familia ya Kambare, mtoto ndevu na baba ndevu, wote wababe.
Na ikumbukwe kuwa kama Simba itapoteza dhidi ya Al Ahly na Yanga basi hata hivyo viporo vitaliwa kwa presha kubwa na huenda ikapelekea kupaliwa.