Kuna vingi vya kukumbuka sana kwenye dunia yetu hii ya mpira. Dunia ambayo haijawahi hata siku moja kupata mwanga.
Dunia ya giza. Giza limefunika mboni za maisha yetu. Tunaenda tu bila uelekeo wowote kwa sababu ya kukosa mwanga wa kutoa giza letu.
Tunaishi tu kwa sababu MUNGU kapenda kuweka pumzi kwenye miili yetu, lakini hatujawahi kabisa kufikiria kwanini MUNGU anatuwekea pumzi kwenye miili yetu.
Akili zetu zimelala sana kwa sababu ya giza kubwa ambalo lipo kwenyrkwenye kwenye dunia yetu hii ya mpira. Giza ambalo linatufanya tuone kila muda ni usiku.
Tunafurahia sana haya maisha, hakuna ambaye anataka kubadilika. Kuanzia viongozi ambao tunawapa dhamana ya kuongoza mpira wetu.
Ugonjwa huu umekuwa ugonjwa wa kuambukiza, viongozi wetu bado wamelala sana, wachezaji wetu nao wamelala sana, tena usingizi wa pono.
Usingizi ambao huwachelewesha wao kufika sehemu kubwa ya mafanikio na mwisho wa siku sisi hubaki kusema fulani alikuwaga na kipaji sana!
Yuko wapi Haruna Moshi “Boban”?, ana mafanikio yapi ya kuigwa na kizazi kipya cha mpira wetu?, hapana shaka hana kitu kikubwa kulingana na kipaji chake.
Kipaji chake kilikuwa kikubwa sana, kipaji ambacho hakikustahili kabisa kukanyaga viwanja vibovu vyetu.
Kipaji ambacho hakikustahili kabisa kucheza ligi yetu hii ambayo ina waamuzi wa hovyo kabisa katika dunia hii.
Kipaji hiki muda huu kilitakiwa kiwe kinajivunia makubwa kutokana na kipaji chake. Leo hii yuko wapi?, Yanga?, ana nini kikubwa cha kumpa moyo hata Fei Toto?.
Kipi kinampa moyo Fei Toto apigane kila akimuona Haruna Moshi ” Boban”?. Hapana shaka hakuna kitu kikubwa kabisa kinachomfanya apigane kila akimuona Haruna Moshi “Boban”.
Mafanikio makubwa ya Haruna Moshi ” Boban” kucheza katika soka la kulipwa kwa kiwango cha juu yalitakiwa kuwa kama chachu ya kupigana kwa kina Fei Toto.
Na wao watamani kufika mbali, lakini imekuwa kitu cha kawaida tu. Haruna Moshi Boban anaonekana wa kawaida tu mbele ya jicho la kina Fei Toto.
Wanamuona kama mtu ambaye hakufanya kitu kikubwa kulingana na kipaji chake alichokuwa nacho. Kipaji ambacho wengi walikihusudu sana.
Leo hii tunaumia kwa kipaji hiki kutofika mbali sana. Hadithi za maumivu kwetu sisi kimekuwa kitu cha kawaida sana katika maisha yetu ya soka.
Leo hii binafsi ninaumia sana kutomuona Mrisho Khalfan Ngassa kutofika sehemu kubwa ya mafanikio ya maisha yake ya mpira.
Hiki kilikuwa kipaji bora kabisa kuwahi kutokea katika dunia yetu ya mpira. Kipaji ambacho kilikuwa kinastahili kucheza ligi yoyote duniani.
Ndiyo!, ligi yoyote duniani ilikuwa inauwezo wa kuipokea miguu ya Mrisho Khalfan Ngasaa. Kwanini?, jibu ni moja tu.
Mrisho Khalfan Ngassa alikuja wakati ambao aina ya wachezaji kama yeye walikuwa wanahitajika sana katika dunia ya mpira.
Wakati ambao dunia ya mpira ilikuwa inahitaji wachezaji ambao walikuwa wanauwezo wa kufunga wakitokea pembeni mwa uwanja.
Wakati ambao kizazi cha kina Ronaldo De Lima kinazikwa na kufufuliwa kizazi cha kina Cristiano Ronaldo.
Hakukuwa na haja tena kutegemea mshambuliaji halisi wa kati kufunga. Tena hawa watu walikuwa wanapigwa vita kutoweka.
Ni moja ya viumbe ambao wametoweka sana mpaka sasa, kuna wakati mwingine makocha wanatumia mpaka viungo wa kati kucheza kama namba tisa muongo “false 9”.
Turudi kwa Mrisho Khalfan Ngassa sasa, huyu ndiye alikuwa kwenye kizazi cha Cristiano Ronaldo. Kizazi ambacho kilikuwa kinategemewa kwa kufunga na kutoa pasi za mwisho.
Kizazi ambacho kilikuja kutusahaulisha kuwa dunia iliwahi kuwategemea washambuliaji halisi wa kati katika suala la kufunga.
Ndiyo maana ilikuwa virahisi kwa Westham United kumwihitaji Mrisho Khalfan Ngassa kwa sababu moja tu, alikuwa mchezaji wa kisasa.
Mchezaji ambaye dunia ya kisasa ya mpira ilikuwa inamwihitaji sana. Lakini alikosa watu sahihi aliochagua wamzunguke.
Hawakuchukua majukumu yake vizuri kumfanya apigane zaidi ili afike mbali. Kitu hiki alikuwa nacho pia Haruna Moshi ” Boban “.
Hakuwa na washauri wazuri wa kumfanya apate njaa ya kupigana zaidi na zaidi. Na kitu hiki na kiona pia kwa Shiza Kichuya.
Kipaji ambacho kimezungukwa na watu ambao hawampi njaa ya kupigana. Kipaji ambacho kinaendana na dunia ya kisasa ya mpira.
Kichuya anahitajika sana na hii dunia ya mpira, anahitajika sana kama kina Boban na Ngassa walivyokuwa wanahitajika, lakini cha kusikitisha ni kuwa, pamoja na mfanano wa miguu wamefanana na akili!.