Sambaza....

Uongozi wa klabu ya soka ya Azam ya jijini Dar es Salaam umethibitisha kumuuza mchezaji kinda wa timu hiyo Yahya Zayd kwenye klabu ya Ismailia inayoshiriki ligi kuu soka nchini Misri.

Taarifa ya klabu hiyo kupitia kwa Jaffary Idd Maganga imesema Yahya ameondoka Jumapili kuelekea Misri ambapo atapimwa afya kabla ya kukamilisha mazungumzo ya kumuuza kinda huyo ambaye pia amekuwa akiichezea timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.

“Ni kwamba Yahya amesafiri kuelekea nchini Misri na amekwenda kwenye klabu ya Ismailia ambayo ni moja ya klabu kongwe Afrika, ambayo imeshiri na kuchukua mataji ya Afrika mara kadhaa,”

“Niwaambie tu watanzania kuwa hajakwenda kwa Mkopo wala hajakwenda kwa ajili ya majaribio, Yahya anakwenda kwenye klabu ya Ismailia kucheza, lakini atafanyiwa kwanza vipimo vya afya baada ya hapo taratibu nyingine zitaendelea, na mazungumzo baina ya vilabu yamekwenda vizuri” amesema.

Afisa Habari wa Azam FC -Jaffary Idd Maganga.

Yahya anakuwa mchezaji wa pili ndani ya muda mfupi kutoka Azam kujiunga na timu za nchini Misri baada ya kiungo Himid Mao kujiunga na Petrojet mwaka jana, jambo ambalo Maganga anasema kuwa linaongeza nguvu kwenye timu ya Taifa hivyo vilabu visiwabanie wachezaji pale wanapokuwa wamepata nafasi ya kupata timu nje ya Tanzania.

Sambaza....