Najua kuna wengi watakuwa wanailaumu sana Yanga kwa kitendo chake cha kupeleka kikosi kilichojaa vijana kwenye michuano ya kombe la mapinduzi.
Kuna wengi wameudhika mno, tena kuna wakati mwingine wanatukana mno na kama kungekuwa na uwezekano wa wao kuwa wanaishi na viongozi wa Yanga wangewapiga ngumi.
Sababu ni moja tu, wamepeleka watoto kwenye kombe la mapinduzi!, watoto ambao walifundishwa mpira jana na Azam Fc.
Watoto ambao wanaonekana hawana ushindani mkubwa kwenye michuano hii. Hawapewi nafasi sana kuchukua kombe hill.
Kitu ambacho kinawauma sana mashabiki wa Yanga. Mashabiki ambao hutamani kubeba kila kitu ambacho kinachokuja machoni mwao.
Kwao wao neno “kushinda” hutembea kwenye mishipa ya damu. Kwa kifupi neno “kushinda” kwao wao ni kama mapigo ya moyo kwenye moyo.
Kila kombe kwao ni muhimu hata kama kiuhalisia halina umuhimu kwao. Kombe la mapinduzi halina umuhimu na halijawahi kutengenezwa lionekane kama muhimu.
Zamani tuliwahi kuwa na kombe la muungano. Kombe ambalo lilikuwa na sura ya muungano kwa sababu tu lilikuwa linashirikisha timu za kutoka “bara” na “visiwani”.
Na siyo kushirikisha tu hizo timu za kutoka ” bara” na “visiwani”, pia mshindi wa kombe hili alikuwa anapata nafasi ya kutuwakilisha kwenye mashindano ya CAF.
Hapa ndipo umuhimu wa kombe la muungano ulipokuwa unaanza kuonekana. Timu zilikuwa zinajiandaa vizuri kwa ajili ya kombe hili.
Timu zilikuwa zinapeleka vikosi vyenye ushindani kwenye hii michuano. Unajua sababu ni nini?, sababu ilikuwa moja tu, kombe hili lilipewa umuhimu.
Kombe hili lilijengwa ili lionekane muhimu kwa vilabu. Ilikuwa ngumu vilabu kupuuza kombe hili kwa sababu ndilo kombe ambalo lilikuwa linampata mwakilishi wetu kwenye michuano ya CAF.
Kocha ataanzaje kuwashauri viongozi wapeleke kikosi dhaifu kwenye michuano kama hii?, michuano ambayo ukishinda unaenda CAF?.
Hawezi hata kidogo kushauri huo upuuzi na badala yake atafikiria namna ambavyo anaweza kuifanya timu yake ishinde hiyo michuano.
Na hii ni kwa sababu moja tu ” umuhimu” wa kombe husika. Kitu ambacho kombe la mapinduzi hawajafanikiwa kwenye hili.
Miaka mingi sana wanaandaa, lakini hawajawahi kufanikiwa kuifanya michuano ya kombe la mapinduzi kama michuano muhimu ambayo kila klabu kutamani kushiriki.
Kuna wakati hii michuano ilikuwa na sura ya Ki-Africa Mashariki. Timu kutoka Afrika Mashariki ziliweza kushindana.
Angalau huu wakati ilionekana kuna tija kwa vilabu kupeleka vikosi imara kwenye michuano hii ili kuitumia kama maandalizi ya michuano ya kimataifa.
Jambo ambalo lilionekana jema. Na kipindi hicho ligi yetu ilikuwa na mechi chache sana , makocha wengi waliona michuano hii itakuwa ni mizuri kwa wachezaji kuendelea kupata mechi nyingi.
Lakini muda huu ni tofauti kabisa, ligi yetu ina mechi nyingi sana. Mechi 38, mechi ambazo zinatoa bingwa, bingwa ambaye ataiwakilisha nchi kwenye michuano ya CAF.
Pia kuna michuano ya kombe la chama, michuano ambayo mshindi ataiwakilisha nchi katika mechi za kombe la shirikisho barani ulaya.
Kwa kifupi kwa sasa kuna michuano ambayo imejengewa sura ya umuhimu kuliko michuano ya kombe la mapinduzi.
Na hapa waandaaji wa michuano hii wamechelewa kuona hili. Najua nchi yetu hutoa wawakilishi wawili tu kila upande(upande wa bara na visiwani) kwenye michuano ya CAF.
Ni ngumu sana kwa michuano ya kombe la mapinduzi kuwa moja ya kombe ambalo linatoa mwakilishi wa nchi kwenye michuano ya CAF ili kuongeza umuhimu.
Najua hilo ni jambo lisilo wezekana kabisa. Lakini kujenga umuhimu wa timu hauishii hapa tu. Africa Kusini wana michuano mingi sana, na michuano mingine haitoi wawakilishi wa nchi kwenye michuano ya CAF.
Lakini timu huchukulia michuano hiyo kwa umuhimu mkubwa kwa sababu moja tu waandaaji wa michuano hiyo wametengeza mazingira ambayo vilabu huona michuano husika ni muhimu.
Waandaaji hutumia muda mwingi sana kuiendesha kibiashara michuano yao. Hutumia muda mwingi sana kubisha hodi kwenye milango ya maofisi mbalimbali wakiwa na bahasha zao mkononi wakiomba udhamini.
Huifanya michuano husika iwe na picha ya ukubwa sana. Ukubwa ambao utasababisha mashabiki wengi waione michuano hiyo kama bidhaa.
Bidhaa ambayo watainunua , tena bidhaa ambayo wakiacha kuinunua lazima wajihisi kuugua.
Kwa kifupi waandaji huuza hisia kwanza kwa mashabiki kiasi cha kuifanya michuano iwe na msisimko. Msisimko ambao huwawezesha waandaji kupata wadhamini kwenye michuano hiyo.
Wadhamini ambao huweka pesa nyingi, pesa ambazo vilabu huona siyo virahisi kuziachia. Hapo ndipo umuhimu wa mashindano huanzia hata kama mashindano husika hayatoi mwakilishi.
Kombe la mapinduzi ni nembo, ni bidhaa ambayo kama ikitafutiwa aina ya uendeshwaji itakuwa ina thamani kubwa sana.
Inatakiwa michuano hii iendeshwe kibiashara, watu waweke pesa zao hapo. Wahakikishiwe kabisa watanufaika vizuri kila wakiweka pesa zao.
Naamini waandaaji wa michuano hii hawajafanya kitu bado. Ndiyo maana michuano hii inaonekana ya kawaida, inaonekana kama bonanza ndiyo maana hata Yanga wamepeleka kikosi dhaifu kwa sababu hawajaona “umuhimu”.