Sambaza....

Karibu katika muendelezo wa  makala maalumu za klabu Bingwa Barani Afrika. Tovuti hii itakuletea mfululizo wa makala hizi hasa kuziangazia timu zote wapinzani wa timu ya Simba SC kutoka hapa hapa nyumbani “TANZANIA”.

Lengo hasa ni kuwajua wapinzani wa mabingwa hao wa Tanzania bara msimu 2017/18 katika hatua hii ya makundi ambapo Simba imepangwa katika kundi D. Kundi hili linahusisha timu nne, AS Club Vita, Simba, JS Saoura na Al-Ahly. Huku mechi ya kwanza inatarajiwa kuchezwa Januari 11, Huku Simba Sc ikianzia nyumbani kukwaana na  JS Saoura ya Algeria katika uwanja wa taifa.

JEUNESSE SPORTIVE DE LA SAOURA  (JS SAOURA).

Kwa kifupi unaweza kuiita JS Saoura au JSS. Hii ni klabu inayopatikana Algeria, katika mji wa Meridja katika jimbo la Bechar.

Klabu hii change ilianzishwa mwaka 2008, rangi kuu za klabu hii ni Njano na Kijani. Uwanja wake wa nyumbani unaitwa Stade 20 Aout 1955 wenye uwezo wa kubeba mashabiki wapatao 20,000 pekee ikiw ni mara tatu ya uwanja wa taifa wa Dar Es Salaam.

Rais wa klabu hii anafahamika kwa jina la Mohamed Zerouati, huku kocha mkuu wa klabu anaitwa  Nabil Neghiz, ikiwa ni klabu yake ya 11 kuifundisha kama kocha. Pia Alisha wahi kuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Algeria mwaka 2014-2017. Na huu ni msimu wake wa kwanza akiwa na JS Saoura kama kocha mkuu baada ya kuitumikia Ohod ya Saudi Arabia msimu wa 2017/18. Kocha huyu anakuwa ni kocha wa 21 tangu klabu hiyo kuanzishwa mwaka 2008.

JS Saoura inashiriki ligi kuu nchini Algeria inayofahamika kwa jina la Ligue Professionnelle 1, na kumaliza katika nafasi ya pili katika msimu huu ulioisha wa 2017/2018 na kuwafanya washiriki Klabu Bingwa Afrika.

SAFARI YA JS Saoura HADI KUFIKIA HAPA KWA MASHINDANO YA ALGERIA.

Klabu hii kwa hapa Tanzania unaweza kuifananisha na Azam Fc japo kila moja ina tofauti kwa mwingine. Kama tunavyojua hatua za timu kufikia hatua ya mwisho ya mashindano katika nchi ni mchakato.

JS Saoura ilitakiwa kuruka viunzi vinne kabla ya kuifikia ligi kuu nchi humo.

 Mwaka 2008-2009 ilishiriki mashindano yaliyo chini ya ukanda (mkoa) na kushika nafasi ya kwanza na kuwafanya washiriki ngazi inayofuata mwaka  2009-10  ligi ya kanda (mikoa) mbalimbali na kubeba kikombe katika ligi hiyo, na kuwavusha hadi mashindano ya ngazi ya taifa , kwa Tanzania ni sawa na ligi daraja la pili mwaka 2010-11, huko nako walibeba ndoo, na kuwavusha hadi ligi daraja la upili (Algerian Ligue Professionnelle 2) na kushika nafasi ya pili na kuwafanya kufuzu hadi ligi kuu nchini humo, na kushika mshindi wa pili kwa mara mbili, msimu wa 2015/2016 na 2017/2018, na kuwafanya washiriki mashindano haya makubwa Afrika kwa ngazi ya vilabu.

Safari ya JS Saoura hadi kufikia hatua hii klabu bingwa Afrika.

Katika hatua ya awali ya mashindano haya , JS Saoura ilicheza dhidi ya SC Gagnoa ya Ivory Coast, na kuichapa jumla ya magoli 2-0. Mechi ya kwanza JS Saoura iliibuka na ushindi wa 2-0 uwanja wa nyumbani na ugenini walitoka sare tasa. Mechi ya raundi ya kwanza JS Saoura ilicheza na Ittihad Tanger ya Morocco, bila shaka unaikumbuka timu hii ndio ilicheza mchezo wa kirafiki na Simba ikiwa nchini Uturuki. Tanger walikubali kulala kwa jumla ya magoli 2-1, mchezo wa nyumbani walishinda 2-0 na ugenini walifungwa 0-1 na kuwafanya wasonge mbele kwa tofauti hiyo.

Mpaka JS Saoura inaingia katika hatua ya makundi ikiwa na jumla ya goli 4 wao wakiruhusu goli 1 pekee ugenini. Hawajawahi fungwa wakiwa uwanja wao wa nyumbani katika mashindano haya.

Magoli hayo manne yamefungwa na Hammia  goli 2 (kwa penati), Boulaouidet 1 (penati) na  Konate 1.katika michezo yote mine ya hatua ya awali nay a kwanza.

Kwa takwimu hizi, JS Saoura wanaonekana hawana safu kali ya ushambuliaji, wana safu nzuri ya ulinzi na wanacheza kwa mipango kutokana na uhitaji wa mechi.

HALI YA KIKOSI.

JS Saoura ina jumla ya wachezaji 26 pekee wenye wastani wa miaka 27.5. Kati ya hao, wachezaji kutoka nje ya Algeria ni watatu pekee, ambayo ni sawa na 11.5% pekee ya kikosi kizima.

Katika mechi yao ya mwisho ugenini dhidi ya Tanger, walitumia mfumo wa 4-5-1 wakilenga kujilinda zaidi. Na kikosi kilichoanza kilikuwa na wachezaji wafuatao:

Nateche alianza golini akiwa pia kama nahodha, beki wa kulia Khoualed, kushoto Bekakchi, wa kati ni Boubekeur na Talah. Viungo wawili wakabaji, Merbah na Bouchiba na mmoja akishambulia ambaye ni Hammia. Viungo wa pembeni (mawinga) kulia alianza Zaidi na kushoto alikuwepo Koulkheir, na mshambuliaji wa mwisho alikuwa ni Boulaouidet.

Katika benchi walikuwepo wachezaji saba ambao ni golikipa Khaled Bookacem, mabeki, El Hadji Youssoupha Konate na Ahmida Zenasni, Viungo Sid Ahmed Aouedj, Nabil Bousmaha, na Yahia Cherif na mshambuliaji Moustapha Djallit.

Katika kikosi chote cha JS Saoura, akiwemo Mtanzania, Thomas Ulimwengu, hakuna mchezaji aliyefunga zaidi ya goli 5 katika msimu huu wa ligi nchini Algeria. Anayeongoza kwa magoli klabuni hapo ni M. Hammia (Kiungo mshambuliaji) ana goli 4, M. Boulaouidet na M. Djallit( washambuliaji) magoli 3, H. Zaidi (winga wa kushoto) goli 2, E. Konate, beki kutoka Ghana ana magoli 2.

JS Saoura inaonekana kuwa ni timu ya kawaida katika kundi hili. Timu hii itakutana na Simba SC katika mchezo wake wa kwanza hapa Dar Es Salaam utakaochezwa januari 11 mwaka 2019.

Sambaza....