Sambaza....

Katika ulimwengu wa Soka, ukisikia  jina la “Jose Mourinho”  kuna picha nyingi zinakujia kichwani, na picha hizo zinategemeana na jinsi unavyomkumbuka mreno huyo  kwa kile alichoifanyia timu yako  au kwa jinsi unavyolijua soka la dunia  tangu akiwa Fc Porto na vilabu vingine.

Mreno Jose Mourinho alizaliwa mwaka  1963, januari 26 yaani kwa sasa ana miaka  56 kasoro siku kadhaa tu na hadi sasa Mourinho anaifundisha Man U  ikiwa ni msimu wake wa 10 katika ligi ya Uingereza akiwa ameshinda mataji  3 ya ligi hiyo akiwa na Chelsea katika msimu wa 2004/2005, 2005/2006 na 2014/2015 kabla ya kutimkia  kwa Mashetani wekundu, Manchester United.

Kibongobongo jina la Mwinyi Zahera “ Papa Zahera” bila shaka nalo ukilisikia kuna kitu kinakujia kichwani haraka haraka. Kwanza ni kocha wa Yanga, pili anajua kuongea kile anachokiamini kuwa ni ukweli kutokana na hali halisi.

Zahera, Kocha wa Yanga

Mwingi Zahera alizaliwa mwaka  1962, oktoba 19 yaani ana miaka  56, mchezaji wa zamani wa  club DC Motema Pembe , ana uraia wa nchi mbili Ufaransa na Congo.

Yanga inakuwa ni timu ya tatu kwake akiwa kama meneja , baada ya   DC Motema Pembe,  AFC Tubize,  na timu ya taifa ya DR Congo ambayo hadi sasa bado anahudumu kama kocha msaidizi.

Tabia na mienendo inayoendana ya makocha hawa wawili  unaweza hata kuwaita ni mapacha wasiofanana kwa maana wana sifa  kuu ambayo inawaunganisha wote kwa pamoja  lakini kwa muonekano wa nje wako tofauti.

Kwa muonekano wa ndani makocha hawa wote ni waongeaji, yaani wanakiongea kile wanachoamini ni ukweli, wanajiamini na kujituma kwa ajili ya wachezaji wao.

Zahera amelidhihirisha hilo mara kadhaa. Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wachezaji  akiwemo golikipa Beno Kakolanya na beki kisiki, Kelvin Yondani juu ya kutopata stahiki zao kwa wakati, na Zahera amekuwa mkweli hata mbele ya waandishi wa habari kwa kuitaka klabu yake kumalizana na wachezaji hao mapema  ili mambo mengine yaendelee. Sio hivyo tu pia hupenda kujidhihirisha kuwa yeye ana mamlaka kama kocha hataki kuingiliwa kwenye majukumu yake na hata misimamo. Mfano mzuri ni sakata la kurejea kwa Beno kama kipa hali ya kuwa alionyesha utovu wa nidhamu kwa kocha huyo kwa kutohudhuria mazoezi. Msimamo wa kocha huyo ni kwamba kama Beno atarudi itambidi yeye aiache Yanga.

Mourinho kwa upande wake, amekuwa na tabia hii kwa takribani timu zote alizofundisha kiasi cha kumuita “ Mbwatukaji” hii haina maana kuwa Mourinho alikuwa akiongea uongo bali anaongea vile vitu ambavyo wengine hawawezi kuvisema hadharani. Si kitu cha kushangaza kumsikia Mourinho akiwaponda viongozi wa Man U kwa kutofanya usajili kwa wachezaji anaowata, na wakati mwingine huwambia ukweli hata mashabiki wa timu hiyo kuwa wasitegemee chochote na aina ya kikosi alichokuwanacho.

MANCHESTER, ENGLAND – OCTOBER 02: Jose Mourinho, Manager of Manchester United gestures prior to the Group H match of the UEFA Champions League between Manchester United and Valencia at Old Trafford on October 2, 2018 in Manchester, United Kingdom. (Photo by Michael Regan/Getty Images)

Zahera hawaogopi wachezaji, huwaambia ukweli. Bila shaka utakubaliana na mimi kwa hili, si kazi ngumu kumsikia Zahera akimtaja Ibrahim Ajibu, Tshishimbi na Kindoki kucheza chini ya kiwango katika mchezo husika  wala hawaogopi. Wakati makocha wengine kama Jurgen Klopp wa Liverpool mara kwa mara huwatetea wachezaji wake wanapokosea.

Mourinho kwa hili naye hajambo. Ni rahisi sana kumchana makavu mchezaji yeyote hata kama ndie staa wa timu. Mchezaji kama Paul Pogba, Lukaku na Antonio Martial huambiwa ukweli mbele ya kamera kama wamecheza chini ya kiwango kwenye mchezo husika.

Saikolojia kwa wachezaji. Zahera anaonekana kuijua saikolojia ya wachezaji nje ndani. Tuikumbuke Yanga aliyoiacha George Lwandamina, Yanga ambayo  ilikuwa ni rahisi kufungika hata na timu za kawaida, nakumbuka katika michezo ya mwisho ya ligi msimu  2017/2018 Yanga ilipoteza mechi 6 na kupata sare kadhaa.

Ujio wa Zahera ulionekana hauna tija kwa kuwa timu ilikuwa katika  matatizo makubwa ya kiuchumi. Kocha aliituliza timu, alikutana na wachezaji wote na kuamua kazi ianze, na kambi ikawekwa Morogoro.

Bila shaka hata yeye ana stahiki zake lakini anajua jinsi ya kuishi katika mazingira kama ya Yanga  na  bado akainufaisha kwa kuipatia ushindi kwa kila mechi atakayoisimamia kama kocha.

Kwa upande wake Mourinho, aliikuta Man U ikisota chini ya Luis Van Gaal lakini baada ya  kuingia yeye msimu wa 2016/17  na kuisaidia timu kumaliza katika nafasi nne za juu, akabeba kikombe cha Europa na kubeba ngao ya jamii, na msimu uliopita alishika nafasi ya pili chini ya mabingwa Man City na kwa sasa anafanya vizuri katika ligi ya mabingwa barani ulaya kwani Man U tayari imeshafuzu  katika hatua ya mtoano na itakutana na PSG ya Ufaransa .

Wazee wa mechi kubwa. Mourinho “hapendi dharau” unaweza ukasema hivyo. Michezo yote muhimu  kocha huyo hufanya kitu ambacho wengi wanashindwa kukiamini. Licha ya kupoteza dhidi ya Liverpool lakini rekodi zinaonesha Mourinho hushinda mechi hizo ( Big Match). Nakumbuka msimu uliopita, Man City walitakiwa kutangaza ubingwa baada ya kumfunga  Man U, lakini Pogba alikuwa mwiba na kuwashangaza wengi. Mourinho kwenye mechi kubwa si wa kumdharau hata kidogo.

Nikihamia upande wa Papa Zahera haraka haraka picha ya watani wa jadi inanijia kichwani, ikiwa ni msimu wake wa kwanza katika ligi kuu Tanzania bara, mechi yake ya kwanza kukaa katika benchi la Yanga kama kocha mkuu, Zahera aliwashangaza wengi, kwani alijua Simba inauwezo mzuri wa kumiliki mpira, na akaamua kuwaachia umiliki wa mpira, lakini baada ya dakika 90, mechi iliisha kwa sare tasa.

Ni dhahiri kuwa makocha wote ni wazuri wa kusoma mbinu za mpinzani na kuja na mfumo utakaowapa matokea kwa namna yoyote ile. Licha yakufanana huko pia yapo mengi wanayotofautiana kama makocha,je kwa ufanano huo  inatosha kuwaita makocha hawa mapacha?.

Sambaza....