Shirikisho la soka nchini ‘TFF’ limendesha kliniki ya kusaka vipaji vipya kwa vijana iliyofanyika kwenye uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza, kliniki ambayo imeendeshwa na kusimamiwa na Mkurugenzi wa ufundi, Ammy Conrad Ninje na kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania Emmanuel Amunike.
Kliniki hiyo ambayo imehusisha vituo vya kulea na kukuza vipaji kwa watoto kanda ya ziwa, imehusisha zaidi ya vijana 300 ambayo itaendelea kwa siku mbili Jumapili na Jumatatu, ikiwa na lengo la kutafuta wachezaji wa kujazia kwenye timu ya vijana itakayoshiriki kwenye michuano ya Afrika chini ya umri wa miaka 17 itakayofanyika hapa nchini mwakani.
Kocha wa Taifa Stars Emmanuel Amunike ameisifu TFF kwa kuanzisha program hiyo ambayo mbali na Mwanza pia itafanyika jijini Arusha, kwa kusema kuwa hilo litasaidia kujenga timu bora ya Taifa ambayo itashindana kwenye michuano ya AFCON.
“Hiki ni kitu kizuri ambacho TFF wanakifanya, niliwahi kuwa mpango huu nikiwa timu ya Nigeria, kama unavyoona kwa sasa Nigeria imekuwa na vijana wengi kwenye timu za Taifa, hili naliona pia hapa, vijana wamekuwa na moyo wa kujifunza na kuonesha kile ambacho wanacho wengi wamekuja hapa toka saa 12 asubuhi kujaribu bahati yao ni kitu kizuri na kinaweza kuijenga timu bora ya Taifa baadae,” amesema Amunike.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF Ammy Conrad Ninje akataja sababu ya kuichagua kanda ya ziwa kufanya Kliniki hiyo, akisema kuwa namna maumbo ya urefu na nguvu ya vijana wengi wa Mwanza ndio chachu ya wao kuichagua Mwanza.
“Nimekaa Tanzania muda mrefu na najua huku Tanzania mnatengeneza wachezaji wenye nguvu, kwa hiyo kwenye mkatati wa kuchagua wachezaji nilioutengeneza tulikuwa tunahitaji wachezaji wenye nguvu, maumbo makubwa na wanaojua kucheza mpira na tutakuwa tunakuja mara nyingi huku kuendesha semina mbalimbali,” amesema.
Kliniki hiyo itaendelea mpaka Jumatatu ambapokwa mujibu wa Mwenyekiti wa chama cha soka mkoa wa Mwanza Vedastus Lufano, wachezaji watano pekee ndio wanaotafutwa kwa ajili kuongezwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Boys).