Sambaza....

Shirikisho la soka nchini TFF limekanusha Taarifa ya ubadhirifu wa fedha takribani shilingi Milioni 300 zilizochapishwa na gazeti moja hapa nchini.

Katika taarifa hiyo iliyoandikwa na Afisa Habari Clifford Mario Ndimbo imesema Kuwa kiasi hicho kilichotajwa na gazeti hilo tayari zipo katika sehemu husika na wala si mpya kama wadau wa soka walivyodhani ama kuaminishwa.

“Taarifa hiyo imejikita kwenye Taarifa ya Hesabu za TFF za mwaka 2015 na 2016 zilizopokelewa tarehe 11 Septemba 2016 na tarehe 27 Novemba 2017 kwa mfuatano na kufanyiwa kazi,” Taarifa hiyo imesema.

“Katika kipindi hicho kilichotajwa kimekuwa chini ya ukaguzi wa PCCB na tayari mashauri yako mahakamani yanaendelea ikiwa ni pamoja na kufuatilia waliotajwa katika hesabu za fedha katika kipindi cha mwaka 2015 na 2016. Kwa kuwa masuala hayo yapo kwenye ngazi ya mahakama, TFF inaona iviachie vyombo vya kisheria vifanye kazi yake kadiri ya taratibu zao,” imeeleza.

Taarifa hiyo iliyochapwa kwenye gazeti la Tanzanite toleo namba 292 la Jumatatu Disemba 10, 2018 ilikuwa na kichwa cha habari “KASHFA TFF, ZAIDI YA 300M/- ZATAFUNWA”.

Sambaza....