Klabu ya soka ya Mtibwa Sugar ‘WanaTam Tam’ ya Manungu Turiani mkoani Morogoro wameanza vyema michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika, baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Northern Dynamo ya nchini Ushelisheli.
Mtibwa Sugar wakicheza kandanda safi kuanzia sekunde ya kwanza ya mchezo katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam walifanikiwa kupata mabao mawili katika kila kipindi cha mchezo huo.
Shujaa wa mchezo huo ulioamuliwa na mwamuzi Pilan Ncube kutoka Zimbabwe ni Jaffary Kibaya aliyefunga mabao matatu pekee yake yaani Hat Trick katika dakika ya 13, 26 na kwa njia ya penati katika dakika ya 58 kabla ya Ismail Aidan Mhesa kukwamisha bao la nne katika dakika ya 90 ya mchezo huo.
Matokeo hayo yanawapa nafasi nzuri Mtibwa kuelekea katika mchezo ujao utakaopigwa Disemba nne nchini Ushelisheli kwani itawalazimu Northern Dynamo kupata ushindi wa zaidi ya Mabao 5-0 ili kusonga mbele.
Aidha wawakilishi wengine katika michuano hiyo kutoka Zanzibar timu ya soka ya jeshi la Zimamoto watakuwa kibaruani kesho nchini Afrika Kusini watakaposhuka kuumana na Kaizer Chiefs, huku usiku Maafande wa JKU wakiwa katika kibarua kizito dhidi ya Al Hilal ya Sudan katika mchezo wa ligi ya Mabingwa Afrika.