Mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Misri Mohamed Aboutrika amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kosa la kukwepa kulipa kodi.
Aboutrika anaweza kukwepa kifungo hicho kama atalipa faini ya Dola 1115.
Aboutrika hakuwepo mahakani Jijini Cairo wakati hukumu hiyo ikisomwa ambapo alikutwa na hatia ya kukwepa kodi ya zaidi ya dola za Kimarekani Elfu 40 kwa kutoa Matangazo ya vinywaji baridi na huduma za mawasiliano kati ya mwaka 2008 na 2009.
Aboutrika ambaye anatajwa kuwa mchezaji maarufu zaidi katika soka la Misri amekuwa akiishi uhamishoni nchini Qatar toka mwaka 2013 akifanya kazi katika kituo cha luninga cha BeIN Sports baada ya mahakama kumuorodhesha kama mtu hatari kwa usalama wa nchini, lakini jina lake liliondolewa katika orodha hiyo Julai mwaka huu.
Licha ya kuondolewa huko lakini Bado Aboutrika anabaki kuwa miongoni mwa Watu 1529 ambao serikali ya Misri inawaangalia zaidi kama watu hatari kwenye usalama wa nchini humo toka April 19, 2013.
Tayari baadhi ya Mali za nguli huyo wa soka zimezuiliwa na serikali toka mwaka 2015 miaka miwili tu baada ya kustaafu soka la ushindani lakini mwaka 2016 mali zake ziliachiwa.