Makamu wa Rais wa klabu ya soka ya AS Monaco Vadim Vasilyev ameendelea kuonesha kumuamini kocha Thierry Henry licha ya kufanya vibaya katika michezo yake sita ya mwanzo toka alipokabidhiwa kibarua hicho.
Vasilyvev amesema hawawezi kumjaza pressure ya kuondoka klabuni hapo kocha huyo ambaye ametoka sare michezo miwili na kupoteza michezo minne toka aliporithi mikoba ya kocha Leonardo Jardim.
“Thierry Henry amekuwa hapa kwa mipango ya muda mrefu, yeye sio mzima moto, hatujawahi kuwa na mahusiano mabaya nay eye, tunajua timu haina wachezaji wengi majeruhi (licha ya kadhaa wa kikosi cha kwanza kuwa na majeraha) lakini imekosa hali ya kujiamini na bahati,” amesema Vasilyvev.
Tayari wachambuzi wengi wa masuala ya soka wamemuweka kiti moto kocha Henry kwa sababu bado hajashinda mchezo wowote na timu imeendelea kufanya vibaya kwani tayari imeshatolewa katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.
Monaco ambao wanashika nafasi ya 19 katika msimamo wa ligi wakiwa na alama 7 katika michezo 13, baada ya kuchezea kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa PSG jana watacheza na Caen siku ya jumamosi katika mchezo ambao unatazamiwa pengine utakuwa wa kwanza kwa Henry kupata ushindi.