Baada ya Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumfungia maisha kutojihusisha na soka aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi TFF, wakili Revocatus Kuuli, mwenye amejitokeza na kubeza maamuzi hayo
Akitaja hukumu hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili TFF, Hamidu Mbwezeleni, alisema wamemfungia wakili huyo kutokana na kukiuka misingi ya katiba ya TFF, lakini Kuuli amesema kuwa hukumu hiyo haina mashiko kwani tayari alikuwa ameshajiuzulu.
Kuuli amesema kamati ya maadili ya TFF ni sawa na Mahakama ya Kangaroo ambayo inafanya maamuzi yasiyofuata sheria na kanuni ambazo wamejiwekea wenyewe na kutoa angalizo kwa TFF kuwa kama wataendelea na misingi hiyo basi itakuwa ni kazi kukuza soka nchini.
“Ni maamuzi ya kipuuzi, hiyo ni mahakama ya Kangaroo, na wala sitarajii hata kukata rufaa, ninaona hayo ni mambo tu ambayo yanapita katika maisha, wapo wengi ambao walipewa adhabu kama hizo na wanaendelea na maisha,”
“Wamenipa tuhuma za kipuuzi na hazina maana yoyote, kwa sababu kitu kinachokatazwa kusambazwa ni kile ambacho kimezuiwa, barua zao wamenitumia kwa email na whatsApp kwa hiyo unaweza kuona sasa hiyo taasisi kile ambacho wanakisimamia hata hakieleweki,” amesema.
“Pale TFF kwa sasa hakuna kitu kikubwa sana na cha maana tunaweza kutarajia kwa sababu ukiangalia vizuri kuna watu wana genge ambalo litaka kunufaina, kuna genge la watu ambao ni wahuni na si makini, tusitarajie maendeleo ya mpira, kwani hata sasa hakuna wadhamini ukiuliza watakuambia kuna watu wanatuhujumu lakini sio kweli,wahuni wamejazana pale,” Kuuli ameongeza
Kuuli alishtakiwa mbele ya kamati ya Mbwezeleni kwa kukiuka misingi ya katiba ya TFF kwa kusambaza nyaraka ya siri aliyetumiwa na Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao hivi karibuni juu ya suala la uchaguzi wa klabu ya Simba.