Nyota wa timu ya Taifa ya Vijana chini ya Umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ Kelvin Pius John ‘Mbappe’ anatarajiwa kuwa nchini Denmark kwa muda wa siku 18 katika Programu ya maendeleo ya kimichezo na timu ya HB Koge inayoshiriki ligi kuu nchini humo.
Wakala wa mchezaji huyo ambaye ni mkurugenzi wa kituo cha michezo cha Bares Sports Academy kilichopo Wilayani Magu Mkoani Mwanza, Jamal Bares amesema program hiyo wanaamini itamjenga Kelvin katika maendeleo yake binafsi.
“Sisi kama kampuni ya usimamizi wa wachezaji tunaamini safari hii itamjenga sana Kelvin katika maendeleo yake binafsi lakini pia katika muunganiko wa timu wa Serengeti Boys, kwa hiyo tunashuruku kituo chake cha Football House kwa kutupa nafasi kwa sababu wengi walituma maombi ya kutaka kumsimamia lakini wakatuchagua sisi,” Baras amesema.
Kelvin ambaye alikuwa mchezaji bora wa mashindano ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati iliyofanyika mwaka jijini Dar es Salaam atakuwepo katika Programu hiyo na klabu hiyo ya HB Koge ambayo inasifika kwa kukuza na kuendeleza vipaji.
“Tunafuraha kubwa kwani tunaamini Kelvin John ni mchezaji wenye kipaji cha hali juu na atakwenda kuipeperusha vyema Bendera ya Tanzania,” Baras amesema.
Mbali na program hiyo lakini Pia Kelvin atapata nafasi ya kufanya Majaribio katika klabu hiyo ambayo inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi kuu nchini Denmark wenye timu 12.