Erasto Edward Nyoni na Feisal Salum “Totó” walibaki kua gumzo kwa mashabiki baada ya ushindi wa mabao mawili ya Tanzania dhidi ya Cape Verde katika dimba la Taifa baada ya kuonyesha kiwango kikubwa katika mchezo ule.
Erasto Nyoni alianza katika eneo lá kiungo wa ulinzi baada ya kukosa mchezo wa kwanza wa ugenini, huku Feisal Salum akiingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Mudathiri Yahya Abas. Wote wawili waliweza kufanya vizuri katika maeneo yao kiasi kwamba kubaki midomoni mwa mashabiki walioutazama mchezo huo.
Gumzo lingine lililobaki ni nafasi walizotumika katika timu ya Taifa chini ya mwalimu Amunike na nafasi zao wanapokua wanatumikia vilabu vyao katika michuano mbalimbali. Feisal Salum amekua akitumika kama kiungo wa ulinzi huku kiraka Erasto Nyoni akitumika kama mlinzi wa kati.
Feisal Salum
Fei Totó amekua akitumika na mwalimu Mwinyi Zahera kama kiungo wa ulinzi huku mbele yake akicheza Pappy Tshishimbi. Lakini mara nyingi amekua akifanya makosa mengi kiasi cha kupeleka kucheza faulo nyingi na kuonyeshwa kadi za njano katika michezo ya Ligi Kuu Bara.
Hivyo basi huenda kupitia mwalimu Emmanuel Amunike, kocha wa Yanga anaweza kushawishika kubadili nafasi na kumtumia kama kiungo wa ushambuliaji anapoonekana kuwa na “Impact” zaidi kwa jinsi alivyo na uwezo wa kupiga pasi na kuchezesha timu.
Erasto Nyoni
Nyoni amekua akitumika kama beki wa kati katika kikosi cha Simba huku “aki-double” na Pascal Wawa. Lakini kurudi kikosini kwa beki wa Uganda Juuko Mursheed kumemfanya mwalimu Patrick Ausems kutamani kumtumia kutokana na aina ya uchezaji wa Wawa na Nyoni kufanana.
Kwa jinsi mwalimu Amunike alivyoweza kumbadili kiraka huyo na kucheza vizuri nafasi ya kiungo wa ulinzi ambayo mara nyingi katika klabu ya Simba imekua chini ya jonas Mkude na James Kotei huenda pia kukamshawishi Mbelgiji kumsogeza katika eneo la kiungo haswa kutokana na majeruhi ya Jonas Mkude na pia kumpa nafasi Juuko Mursheed katika eneo la ulinzi.
Yote kwa Yote walimu wa vilabu hivi viwili ndio wenye maamuzi ya mwisho ya namna ya kuwatumia katika timu zao na kuleta faida katika timu.