MLINZI na ‘kiraka’, Erasto Nyoni amerejeshwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ( Taifa Stars) ambacho kitashuka dimbani kuwavaa Cape Verde Island katika mchezo marejeano kuwania nafasi ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika 2019-fainali ambazo zitafanyika nchini Cameroon.
Kuitwa tena kwa Erasto, upande wangu ni jambo zuri mno kwa maana katika mchezo uliopita siku ya Jumamosi ambao Stars ilichapwa 3-0 jijini Praia kikosi hicho kilicho chini ya kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike kilionyesha kukosa utulivu; uwezo wa kupanga mashambulizi kutokea nyuma ukitia shaka.
Erasto ni mchezaji mwenye uwezo wa kutuliza presha kwa wachezaji wenzake pindi wanaposhambuliwa, ni mzuri pia katika kukaa na mpira na kuanzisha mashambulizi kutokea nyuma-jambo ambalo halikuonekana Jumamosi iliyopita.
Lakini licha ya kumuongeza mchezaji huyo wa klabu ya Simba, ili kufanikiwa kupata ushindi katika mchezo wa kesho, ningemshauri kocha Amunike kufanya maamuzi ambayo pengine upande wake yatakuwa magumu lakini kwa uelekeo wa mchezo huo naamini yatakuwa na faida kubwa kwa Stars.
MFUMO
Mfumo siku zote huchezesha timu na husaidia pale timu inapokuwa ikishambuliwa. Baada ya kupoteza ugenini wikend iliyopita, kocha Amunike anatakiwa kutazama upya aina ya mfumo wake. Katika michezo miwili aliyoisimamia Stars, Mnigeria huyo alitumia mfumo wa 3-5-2 na kufanikiwa kupata alama moja, kuruhusu magoli matatu huku kikosi chake kikishindwa kupata goli lolote katika dakika zake 180 za mwanzo.
Dhidi ya Uganda ilikuwa 0-0 Kampala, na Cape Verde wakainyuka Stars 3-0. Michezo yote hii ilikuwa ni ugenini kwa kuwa atakuwa akiiongoza Stars kwa mara ya kwanza akiwa nyumbani, Amunike anatakiwa kutumia mfumo wa asili ya Tanzania; 4-4-2 ili kuifanya timu kutawanyika na kutengeneza nafasi za kufunga.
MABEKI WANNE
Katika 4-4-2, Amunike anapaswa kufanya mabadiliko makubwa katika ngome yake. Kwanza ni kuwaondoa walinzi watatu aliowatumia katika michezo miwili iliyopita. Hassan Kessy anapaswa kumpisha, Shomari Kapombe katika beki namba mbili, Agrey Morris na David Mwantika wanatakiwa kurudi benchi ili kuwapa nafasi Erasto na Kelvin Yondan.
Kuwapanga, Kapombe, Gadiel Michael upande wa kushoto, Erasto na Kelvin katika beki ya kati kutaifanya Stars kuanzisha vizuri mashambulizi kutokea nyuma. Katika michezo miwili iliyopita, Kessy, Mwantika na Aggrey wote walikosa utulivu hasa kule Praia wakati Stars iliposhambuliwa sana.
VIUNGO WANNE
Abdi Banda ameshindwa kuonyesha kitu tofauti katika michezo miwili aliyocheza chini ya Amunike. Mfumo wa mabeki watatu na viungo watano umeshindwa kumsaidia kiungo huyu mlinzi wa Baroka FC ya Afrika Kusini.
Katika 4-4-2, Banda anaweza kuwa na mchango mkubwa kama atatumika kama kiungo wa ulinzi. Amunike anatakiwa kumsogeza mbele kidogo Mudathir Yahaya, Mudathir Yahaya ambaye licha ya kwamba ni kiungo mzuri lakini si bora katika ukabaji.
Banda anaweza kufanya vizuri akicheza sambamba na Saimo Msuva katika wing ya kulia, Mudathir kama kiungo wa mashambulizi na Thomas Ulimwengu katika wing ya kushoto. Wane hawa wanaweza kumsaidia Amunike na mbinu zake zikafanya kazi vizuri.
WASHAMBULIAJI WAWILI
Kwa miezi 15 sasa John Bocco amekuwa juu kimpira, amepevuka mno na wakati akiwa katika benchi Jumamosi iliyopita alionekana kuwa na usongo wa kuingia uwanjani. Tatizo linguine ambalo lilifanya Stars kushindwa kufanya vizuri Praia ni kukosa mshambulizi ambaye angewafanya walinzi wa kati wa Cape Verde kutoanzisha mashambulizi.
Tom alicheza pembeni zaidi na hilo liliwasaidia watu hao wa Kasskazini Magharibi mwa Afrika kucheza bila ‘buguza’ katika eneo lao la ulinzi. Alipoingia Bocco dakika kumi za mwisho mambo yalikuwa magumu mno kwa wenyeji. Bocco alishindwa kuunganisha vizuri mpira wa krosi ya Shomari na aligongesha nguzo ya goli kwa kichwa cha kujitolea.
Kumpanga Bocco kama mshambulizi namba moja huku nyuma yake akicheza nahodha Mbwana Samatta kunaweza kuipa Stars ‘uhai’ mkubwa katika mashambulizi. Amunike anapaswa kuwaanzisha washambuliaji wake hawa ili timu ipate matokeo ambayo yatawarudisha nafasi ya pili na kufufua matumaini ya kwenda Cameroon hapo mwakani.