Sambaza....

Nchi ndogo ya Gibraltar jana imeibuka na ushindi wa tatu toka ilipoanza kutambulika na shirikisho la soka Barani Ulaya (UEFA) baada ya kuichapa Armenia kwa bao 1-0 katika michuano ya UEFA Nations League.

Nchi hiyo ndogo yenye idadi ya wakazi takribani 32,194 ilikuwa imecheza mechi 22 za ushindani bila kushinda mchezo wowote ikitoka sare katika michezo miwili pekee hadi hapo jana walipoifunga Armenia ya kiungo wa Arsenal Henrikh Mkhitaryan.

Penati ya dakika ya 50 iliyopigwa na nahodha Roy Chipolina ndiyo iliyoipa ushindi huo wa kihistoria nchi hiyo na kukusanya alama tatu kwa mara ya kwanza, katika michuano ya UEFA Nations League, mchezo ambao umefanyika kwenye mji wa Yerevan.

Aidha huu ni ushindi wa tatu toka Gibraltar ilipokubaliwa kujiunga na UEFA mwaka 2013, kwanza wakiichapa Malta mwaka 2014 na mwezi Machi waliichapa Latvia katika mchezo wa kirafiki.

Ushindi huo umekuja baada ya kupigwa kwa wimbo wa Taifa wa Liechtenstein badala ya ule wa Gibraltar kabla ya mchezo huo na tayari Shirikisho la soka nchini humo limeomba radhi kutokana na kitendo hicho.

Toka Gibraltar wajiunge na UEFA wamekuwa mdembwedo wakikubali vichapo vikubwa vikubwa kama kile cha mabao 8-1 dhidi ya Poland, 7-0 dhidi ya Ujerumani, na kichapo kikali zaidi kilikuwa cha mabao 9-0 dhidi ya Ubeligiji mwaka jana.

Sambaza....