Kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Libya Adel Amrouche amejiuzulu nafasi yake ikiwa ni siku chache kabla ya kukutana na Nigeria katika michuano ya kufuzu kwenye fainali ya Mataifa Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Cameroon.
Shirikisho la soka nchini Libya limethibitisha taarifa hizo Jumatano hii, huku Kocha Mbeligiji Amrouche ambaye aliwahi kuwa kocha wa Timu ya Taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’ akisema kuwa mazingira magumu ya kazi ndiyo chanzo cha yeye kuachia ngazi.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 50 ambaye ni mzaliwa wa Algeria alichaguliwa mwezi May kuwa kocha wa Libya na mechi yake ya kwanza alifanikiwa kutoka sare ya 0-0 na Afrika Kusini mwezi uliopita.
Wakati hayo yakijiri Libya italazimika kucheza michezo yake inayofuata kwenye uwanja Huru kutokana na hali ya kiusalama ilivyo kwa nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika, hivyo wataenda kucheza na Nigeria Ijumaa kabla ya kurudiana mjini Sfax nchini Tunisia siku ya Jumatatu
Mpaka sasa Libya wana alama nne kwenye msimamo wa kundi lao wakiwa sawa na Afrika Kusini na wakizidiwa na Nigeria kwa alama moja, huku Ushelisheli akishika mkia kwenye kundi hilo akiwa hana alama yoyote
Ikumbukwe timu mbili kutoka katika kila kundi zitafanikiwa kufuzu kucheza michuano ya Mataifa Afrika inayotazamiwa kuanza mwezi Juni mwakani nchini Cameroon.