Sambaza....

Tangu kuanza kwa wiki hii Maafisa habari wa klabu za Simba na Yanga wamekua wakizunguka mitaani, kwenye vituo vya redio pamoja na kwenye mitandao yakijamii ili kuhamasisha mashabiki wajitokeze viwanjani kwawingi ili kuwapa nguvu wachezaji wao. 

Ahmed Ali kwa upande wa Simba ameonekana katika kampeni hizo katika maeneo ya Tegeta (lilipo tawi la Home Boys) na Msimbazi yalipo makao makuu ya klabu ya Simba lakini pia Ali Kamwe pia aliokuwepo Mbagala katika shughuli ya uhamsishaji wa mashabiki.

Simba atakua na mchezo dhidi ya Raja Casablanca katika mchezo wa kundi C wa Ligi ya Mabingwa wakati Yanga wao watakua na kibarua siku ya Jumapili dhidi ya TP Mazembe katika Kombe la Shirikisho Afrika. Michezo yote hiyo itafanyika katika Dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam. 

Mchambuzi wa soka kutoka kituo cha redio cha EFM Wilson Oruma ametoa maoni yake kutokana na uhamasishaji unaofanywa na vilabu vya Simba na Yanga kuelekea michezo yao ya Kimataifa mwishoni mwa wiki hii

Oruma amesema katika mazingira ya mpira wetu maafisa habari wa Simba na Yanga wapo sahihi kuzunguka mitaani na kwenye vituo vya redio ili kuhamasisha mashabiki kujitokeza viwanjani.

“Katika mazingira yetu tunatakiwa kufanya hivyo, kuhamasishana na kuitana viwanjani. Lakini katika mpira wakisasa huko kwa wenzetu duniani ni wajibu wa shabiki kufika kiwanjani kushangilia timu yake.

Na ndio maana mashabiki huko kwawenzetu ukiona anataka kocha afukuzwe au jambo fulani litokee kwenye klabu yake nikwasababu nayeye anatekeleza wajibu. Unajua shabiki nae ni mwekezaji katika timu, kwa maana ya uchangiaji kama viingilio na kununua jezi,” alisema Wilson Oruma

Nae mchambuzi mkongwe Juma Ayo amesema mashaki wa nchi yetu wanapenda kukumbushwa kutimiza wajibu wao na hivyo kupelekea kampeni kama hizi za na kutumia nguvu ili kuwapeleka viwanjani.

Juma Ayo “Nchi imezoea, tupo kwenye nchi ambayo watu wanahitaji kukumbushwa vitu kila wakati. Lakini pia inaendana na kile kinachotokea uwanjani. Simba na Yanga zote zimefungwa katika michezo yakwanza nasasa michezo hii ya wiki hii ni kama fainali kwao, hivyo wanatumia nguvu kubwa ili kushinda mechi.

Na ikitokea mmoja wapo akafungwa mchezo unaofwata  hata wakienda mitaani mashabiki hawatokwenda tena kwawingi viwanjani. Tupo kwenye nchi ambayo watu wanapenda timu zaidi kuliko mpira, lakini ingekua kwingineko mashabiki wangejitokeza kwawingi kwasababu wanaijua ratiba.” 

Pia Juma aliwasisitiza mashabiki kutimiza wajibu wao kwasababu mpira ni starehe na burudani tosha.

“Mashabiki watimize wajibu wao bila kujali inacheza timu gani, waende viwanjani wachangie timu. Simba kucheza na Raja hiyo ni mechi kubwa mno Afrika wala haiihitaji promo, inajipromote yenyewe. 

Mashabiki watimize wajibu wao sio mpaka wakumbushwe. ” alimalizia Juma Ayo.

Simba itakua uwanjani Jumamosi saa moja usiku kuwakaribisha Raja Casablanca wakati watani zao wao watawaalika TP Mazembe keshokutwa Jumapili saa moja jioni.

Sambaza....