Fainali ya Uruguay na Brazili ya mwaka 1950. Soma mfululizo wa makala hizi kama zilivyoaandaliwa na Maka Mwaisomola. Sherehe zialianza mapema kabisa kwa wabrazili.
Vyombo mbalimbali vya habari na jamii yote ya Wabrazil kwa ujumla tayari walianza kutangaza na kudai kuwa Brazil ndiyo mabingwa wapya wa dunia siku kadhaa kabla ya mechi yenyewe ya mwisho, na walikuwa na sababu ya kufanya hivyo. Brazil walishinda mechi zao mbili za mwisho kwa staili ya kushambulia dhidi ya wapinzani wao ambao juhudi zao zote za kujilinda hazikuzaa matunda.
Hata hivyo, Uruguay, walipata taabu sana katika mechi zao dhidi ya Hispania na Sweden, wakiambulia tu sare dhidi ya Hispania na ushindi mwembamba dhidi ya Sweden. Wakati matokeo haya yalipolinganishwa, ilionekana kuwa Wabrazili watajipanga kuwasambaratisha Uruguay kirahisi kama ilivyokuwa kwa Hispania na Sweden.
Pamoja na hivyo, katika mashindano ya Copa America, ambayo pia yalifanyika Brazil mwaka mmoja nyuma, wenyeji walishinda kwa ushindi wa kushangaza wa mabao 46 katika mechi nane tu. Ecuador waliona hasira za Brazil pale walipochapwa mabao 9–1, Bolivia walichapwa 10—1, wakati ambapo hata washindi wa pili Paraguay hawakuachwa bali walipokea kipigo cha mabao 7–0. Brazil waliendelea kwa kuichapa Uruguay mabao 5–1.
Medali ishirini na mbili za dhahabu zilitengenezwa huku kila moja ikichapishwa jina la kila mchezaji na Meya wa Rio alitoa hotuba yenye maneno haya yafuatayo:
“Nyinyi wachezaji, katika muda wa masaa machache yajayo mtapongezwa kama mabingwa na mamilioni ya wateule! Nyinyi, ambao hamna mpinzani katika ulimwengu wote huu! Nyinyi, ambao mtamshinda mshindani yeyote yule atakayejitokeza mbele yenu! Nyinyi, ambao tayari ninawasalimu kama mabingwa!” Wimbo wa ushindi, “Brasil Os Vencedores” (“Brazil Mabingwa”), ulitungwa na kufanyiwa mazoezi, tayari kabisa kuimbwa na kuchezwa baada ya fainali.
Hata hivyo, Paulo Machado de Carvalho, Mkuu wa msafara wa vikosi vya Brazil vilivyoshinda Kombe la Dunia la mwaka 1958 na mwaka 1962, na ambaye wakati huo alikuwa kiongozi wa São Paulo FC, alifikiria tofauti.
Wakati wa kuitembelea kambi ya mazoezi katika uwanja wa Estádio São Januário kuelekea mkesha wa siku ya mechi, Paulo aliwakuta wanasiasa kibao wakitoa hotuba kwa wachezaji, pamoja na waandishi wa habari, wapiga picha na watu wengine waliofika kujiunga na “mabingwa watarajiwa”.
Wakati alipojaribu kumuonya kocha Flávio Costa kuhusu hatari iliyopo ya kuwafanya wachezaji kutokuweka umakini wa mchezo huo na kuwatoa mchezoni, Paulo hakusikilizwa. Akiwa amekasirika, alimwambia mtoto wake Tuta, ambaye alikuwa pamoja naye: “Tunaenda kupoteza mechi hii”.
Asubuhi ya tarehe 16 Julai mwaka 1950, mitaa ya Rio de Janeiro ilikuwa na pilikapilika. Ngoma aina ya carnival iliyoongezewa vionjo ilitayarishwa, ikiwa na maelfu ya alama zenye kuonyesha kusherehekea taji la dunia, na kuhanikiza kwa sauti “Brazil lazima ishinde!”. Hali ya sauti hizo iliendelea hivyo mpaka karibia dakika za mwisho mwisho za mechi, ambazo ziliujaza uwanja wa Maracanã kwa watu waliolipa viingilio kuhudhuria mechi hiyo idadi yao ikiwa 173,830 na makadirio halisi kukisiwa kuwa zaidi ya watu 200,000. Rekodi hii ya uhudhuriaji wa mashabiki kwa timu moja katika tukio la kimichezo haijawahi vunjwa katika mechi za kimataifa za mpira wa miguu katika viwanja vingi ambavyo mashabiki wake wote wanaweza kukaa katika viti; kwa wakati huo katika uwanja wa Maracanã ulikuwa ni uwanja wa zege usiokuwa na viti.