Sambaza....

MOHAMED Hussein ‘Zimbwe Jr’ ameendelea kutumika katika kikosi cha kwanza cha Simba SC licha ya Mghana, Asante Kwassi kurejea uwanjani kutokana na majeraha aliyoyapata katika mchezo wa ufunguzi wa msimu dhidi ya Tanzania Prisons mwezi Agosti.

Zimbwe Jr- mchezaji bora wa ligi kuu Tanzania Bara msimu wa 2016/17 alitumika zaidi kama msaidizi wa Kwassi msimu uliopita mara baada ya beki huyo wa kushoto kuwasili Msimbazi akitokea Lipuli FC ya Iringa katika usajili wa dirisha dogo mwezi Disemba mwaka uliopita.

Zimbwe Jr amekwishacheza michezo saba kati ya nane ya Simba msimu huu lakini kiuchezaji licha ya kwamnza hajafanya makosa mengi makubwa, ila Simba inaendelea kupungua makali kiufungaji kutokana na kutokuwepo kwa Kwassi.

Zimbwe Jr alipata nafasi kutokana na majeraha ambayo Kwassi aliyapata. Ndiyo amejitahidi sana kupamndisha kiwango chake lakini ukweli mlinzi huyo wa kushoto bado anashindwa kuisaidia timu kupata mabao kama ilivyokuwa upande wa Kwassi ambaye alitengeneza magoli yasiyopungua tisa msimu uliopita.

Mtazamo wa Zimbwe Jr katika ulinzi hautofautiani na ule wa Kwassi lakini shida ya Zimbwe Jr ni kwamba anashindwa kucheza kama kiungo wakati anapoingia katika eneo la kiungo, pia pasi zake za mwisho hapigi moja kwa moja kwa mlengwa, na krosi zake mara nyingi anapiga tu eneo la kati na si kwa mlengwa.

Mtazame Kwassi anaposhambulia, yeye hujigeuza katika na kujitoa katika uchezaji wa kibeki kila anapovuka eneo la kati. Kwassi hupiga krosi au pasi ya mwisho kwa mchezaji husika na si kupiga tu eneo la kati kama afanyavyo Zimbwe Jr.

Kuna watu wanasema Zimbwe Jr karejesha ubora wake, hilo sawa, kwa namna alivyokuwa na kiwango kibovu katika michuano ya Cecafa Challenge Cup kule Nakuru Kenya mwezi Novemba mwaka jana, bila shaka Zimbwe Jr amejitahidi kurudisha ubora wake lakini kwa mchezo wa Simba ulivyokuwa wakati Kwassi akicheza ni wazi timu hiyo inaendelea kuporomoka.

Upande wa kushoto wa Simba ulikuwa chanzo kikuuu cha magoli mengi wakati walipotwaa ubingwa wa ligi msimu uliopita, lakini kwa sasa upande huo umepunguza makali na hauna mchango mkubwa katika uzalishaji wa magoli licha ya kwamba Zimbwe Jr amekuwa akipanda mara kwa mara na kupiga krosi-pasi kadhaa zisizo na mwelekeo sahihi.

ANACHOTAKIWA KUFANYA ZIMBWE JR

Kwanza aelewe amepata nafasi hiyo kutokana na mpinzani wake kuwa majeruhi hivyo ni lazima aendelee kujituma zaidi katika mazoezi wakati huu Kwassi akisubiri nafasi yake katika benchi. Zimbwe Jr anatakiwa kuboresha upigaji wake wa pasi za mwisho anaposhambulia. Anatakiwa pia kupiga krosi zake kwa mlengwa anayekusudia na si kupiga tu eneo la kati kama anavyofanya sasa.

Kwassi anaweza kuwa mwalimu wake mzuri, lazima acheze kama beki wakati akizuhia-jambo hili hapana shaka analitimiza, anatakiwa kubadili mtazamo wake kiuchezaji anapofika eneo la kati- kupiga pasi za uhakika na kuichezesha timu kama kiungop na ipotokea akapata nafasi ya kupiga mpira goli ni lazima afanye hivyo huku akijipa majukumu ya mfungaji.

Mchezaji mzuri ni yule anayebadilika kimtazamo kutokana na maeneo anayokuwepo uwanjani. Zimbwe Jr ni kweli amepandisha kiwamngo chake lakini ameendelea kuifanya Simba kuwa dhaifu upande wa kushoto na siku Kwassi atakapopewa nafasi yake tena tutarajie kumuona Zimbwe Jr akirejea benchi huku Simba ikifunga zaidi kutokea upande wa kushoto.

Sambaza....