Inawezekana ndiye alikuwa mchezaji bora na muhimu katika kikosi cha Simba msimu uliopita.
Aliifanya kazi yake bila kupumzika, kila mechi mguu wake ulikanyaga kila nyasi ya viwanja vyote vilivyoruhusiwa kwa ajili ya ligi kuu Tanzania bara.
Lakini kwa sasa muda umechukua nafasi ya kufanya mabadiliko muda ni nafasi ya mabadiliko.
Na mabadiliko ndicho kitu ambacho maisha hutoa kwa mwanadamu, huwezi kukwepa na kuzuia mabadiliko kama maisha yameamua kutoa nafasi kwa muda, ingawa mara nyingi mabadiliko huja na ukinzani mkubwa
Kinachobaki ni wewe kuchagua kitu kimoja kuangalia muda au kuangalia saa, kwenye muda kila sekunde kuna badiliko jipya hujitokeza wakati mwingine huitaji kuangalia saa kujua muda umekuacha.
Nafasi uliyopo sasa ndiyo hutoa jibu sahihi kuwa muda umekuacha au unaenda sambamba na muda.
Inawezekana msimu jana Mohammed Hussein “Zimbwe jr” alikuwa kwenye nafasi kubwa ya mafanikio lakini changamoto zikaja na upepo wa kumshusha chini ya mafanikio aliyoyafikia na kuwepo kwenye nafasi ambayo anatakiwa kukumbushwa kuwa muda unanyata taratibu kuelekea mbele yake ili umpe kisogo.
Inauma kuona kipaji cha Zimbwe kikiachwa na muda ndiyo maana kuna haja ya kumkumbusha kuwa muda haumsubiri mtu.
Najua kwa sasa anachangamoto kubwa ya kurejea kwenye kiwango baada ya kutoka kwenye majeruhi, lakini changamoto kubwa kwake ni kufanikiwa kumweka benchi Asante Kwasi, mchezaji ambaye amekamilika zaidi kuliko Zimbwe.
Asante Kwasi ambaye anaonekana amepata mambo baada ya kupata fimbo, waweza ukadhani labda fimbo yake aliyoipata anaitumia kumwadhibu Zimbwe kwa sababu ana vitu vingi ambavyo Zimbwe hana
Ushawahi kuwaangalia usoni Zimbwe na Kwasi wanapokuwa wanashambulia? Kuna vitu viwili utaviona kwenye mwili wao, cha kwanza ni kasi kubwa ya Zimbwe dhidi ya ƙkasi ya kawaida ya Kwasi. Cha pili ni utulivu hafifu wa Zimbwe dhidi ya utulivu mkubwa wa Asante.
Pamoja na kwamba Zimbwe anaposhambulia huwa anashambulia kwa kasi lakini hukosa utulivu kama wa Asante anapokuwa anashambulia.
Ndiyo maana maamuzi yao ya mwisho huwa yanatofautiana kwa kiasi kikubwa, mfano msimu jana Zimbwe alifanikiwa kutoa pasi mbili za magoli wakati kwa mechi ambazo amecheza Asante Kwasi akiwa na jezi ya Simba ambazo hazifiki kumi ameshahusika kwenye magoli zaidi ya mawili.
Hii yote inaonesha nani hupania kufanya kitu kizuri na nani hudhamiria kufanya kitu bora, na ndiyo maana Asante kwasi ana magoli 6 kwenye ligi kuu mpaka sasa.
Ni mtulivu anapokuwa katika eneo la kumi na nane, haoni ugumu kujivua sura yake na kujivika sura ya Okwi anapokuwa eneo hili, ni mara chache sana kupata mchezaji ambaye ni beki mwenye uwezo wa kufunga magoli na kutoa pasi za mwisho, hii kwenye mpira ni vitu muhimu vya nyongeza ambavyo Zimbwe hana ingawa akiamua anaweza kuvipata.
Utulivu pekee ndicho kitu kinachokosekana kwenye macho na akili ya Zimbwe, waweza kumuona anahusika kwenye kujenga mashambulizi ya timu lakini linapokuja suala la yeye kutoa maamuzi ya kuzalisha goli kukuangusha ni kitu cha kawaida.
Na ugumu wa kumbeba mbele ya Kwasi ndipo unapoanzia, nafsi yako lazima uiruhusu kumwelewa Kwasi na kumpa nafasi zaidi ya Zimbwe kujifunza.
Yupo kwenye umri wa kujifunza kwa sasa, umri unaompa nafasi ya kusoma mambo mengi ambayo atayatumia kwa baadaye.
Umri ambao haumruhusu yeye kususa kukaa benchi, umri ambao unamruhusu yeye kupigana na kuumia kwanini anakaa benchi?
Umri unaompa nafasi kubwa ya yeye kujihoji maswali mengi ya kwanini?
Kwanini yeye siyo mtulivu anapotakiwa kufanya maamuzi ya mwisho kwenye eneo la hatari la adui( final third)?
Kwanini Kwasi ni mzuri zaidi yake kipindi anapobaki na mshambuliaji wa timu pinzani kumkaba ( one to one battle)?
Kwanini Kwasi huwa anaziba nafasi eneo la beki wa kati kushoto kwa uharaka kipindi ambacho beki wa kati kushoto anapokuwa ameondoka kwenda kutimiza jukumu jingine la ukabaji?
Maswali chanya yanatakiwa yatawale katika kichwa chake, akubali kuipokea hali iliyopo kwa sasa na kutozipa nafasi fikra hasi zitawale katika kichwa chake.
Asikubali kuendelea kusimama, kwani asimamaye haendi mbio, anatakiwa kujua ashapitwa na Kwasi anatakiwa aende mbio na kutoka sehemu ambayo yupo kwa sasa.
Siyo muda sahihi kwake yeye kuanza kulaumu kwanini Mungu aliumba Chui, anachotakiwa kushukuru kuwa Chui hakuumbwa na mabawa kisha aanze kutetea nafasi yake kwa sababu cha mchama huchachama, cha mgura hugura.