Sambaza....

Hakuna mawasiliano ! , Hii ndiyo kauli pekee ambayo unaweza ukaisema kuhusu Mwinyi Zahera na uongozi wa Yanga.

Kukosekana kwa mawasiliano kunawafanya wasiwe na muunganiko kati yao. Ndiyo maana kuna wakati wanafanya vitu ambavyo hawakubaliani kwa pamoja.

Utanishangaa kwa hili, ila subiri nikuambia kitu kimoja naamini utanielewa. Yanga hawana mawasiliano yanayounganisha kati ya timu na klabu.

Tunajua timu inaongozwa na Mwinyi Zahera na Klabu inaongozwa na Dk. Mshindo Msola, katikati ya hawa watu wawili kuna mtu anayeitwa Meneja.

 

Huyu ndiye anayeunganisha timu na klabu. Huyu ndiye ambaye anaweza kutoa tatizo ndani ya timu na kulipeleka kwenye klabu na kurudisha majibu yake tena ndani ya timu.

 

Huyu ndiye muunganishaji wa madaraja haya mawili. Kipi kocha anataka?, matatizo yapi ambayo yapo kwenye timu, vyote hivi vinawasilishwa na meneja.

Ndiyo maana hata mechi za kirafiki za kuelekea mchezo fulani Meneja ndiye huwa anatoa maoni ya kocha ya aina zipi za mechi ambazo zinahitajika kwa sasa.

 

Aina ipi ya viwanjwa vinavyoweza kutumika kwa ajili ya mechi za kirafiki kuelekea mechi husika. Aina ipi ya mji ambao timu inataka kuweka kambi kwa ajili ya kujiandaa na mechi husika.

 

Huyu ndiye anayeunganisha hizi taarifa ili kufanya kitu kiwe kizuri. Yanga walikuwa Kaskazini mwa nchi kwenye mkoa wa Arusha na mji wa Moshi.

 

Walicheza mechi mbili, moja ambayo walifungwa na Polisi Tanzania na nyingine ambayo walishinda dhidi ya AFC Leopards.

 

Tuachane na matokeo yaliyotokea kwenye hizi mechi. Tuwazeni kwa pamoja kuhusu kauli ya Mwinyi Zahera baada ya mechi hizi.

 

Mwinyi Zahera alisema walipoteza muda kuwa Arusha na Moshi. Viwanja ambavyo vilitumika kwa ajili ƴa mechi hizo za kirafiki havikuwa viwanja bora.

Hapa ndipo swali la msingi linapokuja kutokea. Mwinyi Zahera kabla ya kwenda Arusha na Moshi hakuwaambia viongozi wa Yanga aina ya viwanja vinavyohitajika kwa ajili ya mechi za kirafiki ?

 

Hakukuwepo na taarifa inayounganisha haya maeneo mawili kati ya timu na klabu ? Ukitazama vizuri utagundua Mwinyi Zahera na uongozi wa Yanga kila mmoja wanatembea njia tofauti , mwingine akiwa na Baiskeli mwingini na Pikipiki tena wakiwa wamebeba mzigo mmoja!

Sambaza....