Kocha mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema shida ambazo klabu hiyo imekumbana nazo ndizo zimewapa morali ya kupambana na kupata matokeo chanya kwenye michezo ya ligi mpaka sasa.
Zahera amesema wakiwa kambini mkoani Morogoro kabla ya kuanza kwa ligi alikaa na wachezaji wake na kuwaomba kuungana na kuwa wamoja lakini pia kutumia changamoto ambazo wanazo kama fursa ya kupambana zaidi ili kupata matokeo mazuri, na anashukuru kuona hilo limefanyika na sasa wanaongoza ligi.
“Tulipokuwa Morogoro, niliwaita wote na kuwaambia tunatakiwa kuwaza namna moja, mpaka leo unaona tunashinda mechi 16 unaweza kusema ni bahati, hakuna kitu bahati, niliwambia ile tofauti ambayo tunayo tofauti na timu nyingine, na hiyo tofauti ni matatizo yetu, sasa matatizo yetu tunayageuza furaha, hiyo ndiyo kitu ambayo wengi wameshindwa kufanya,” amesema.
Zahera amesema anawashukuru sana wachezaji wake kwa namna ambavyo waliweza kumuelewa toka mwanzo na kubadilisha matatizo kuwa furaha na kufanikiwa kushinda michezo 16 kati ya 18 ambayo wamecheza mpaka sasa kwenye ligi kuu soka Tanzania Bara.
Yanga wanaongoza Ligi wakiwa na alama
50, baada ya kucheza michezo 18 wakifanikiwa kushinda michezo 16 huku mpaka
sasa wakiwa hawajapoteza mchezo wowote licha ya kuwa na ukata wa kifedha.