Jumatatu ndiyo siku ambayo inasubiriwa kukamilisha ndoto ya Phillipe Countinho.
Ndoto ambayo aliipigania kuanzia dirisha la majira ya joto la usajili lililopita lakini Liverpool alipigana kumbakisha.
Walifanikiwa kumbakisha, wakaamini wataendelea kufanya chochote wanachoweza kufanya ili abaki Liverpool.
Lakini jitihada zao zilikuwa bure kwa sababu mwili wa Phillipe Countinho ulibaki Liverpool lakini akili yake ilikuwa Barcelona.
Kila alichokuwa anakifanya, alikifanya huku akiwa ni lini ataenda Barcelona.
Ndiyo maana hakuona hatari kwenda katika kipindi hiki cha usajili wa majira ya baridi.
Hakuona hatari ya yeye kutocheza klabu bingwa ulaya ( UEFA champions League) ili mradi ndoto yake itimie ya kwenda kucheza Barcelona.
Hadithi sasa ishabadirika, Phillipe Countinho yupo katika jiji la Barcelona akisubiri jumatatu afanyiwe vipimo kuona kama atafuzu vipimo awe mchezaji rasmi wa Barcelona.
Ameleta furaha kwa mashabiki wa Barcelona na kuacha huzuni na masikitiko ƙwa watu kwa mashabiki wa Liverpool.
Ameondoka Liverpool , nafasi yake nani anaenda kuiziba?
Hili ndilo swali ambalo tunatakiwa kujiuliza na kutakiwa kulijibu.
Hawa ndiyo wachezaji ambao wanafaa kuchukua nafasi ya Phillipe Countinho pale Liverpool.
Henrikh Mkhitaryan.
Mwaka 2009 aliyewahi kuwa nyota wa timu ya Liverpool, Michel Owen alienda Manchester United akitokea Newcastle United.
Baada ya kujiunga na Galacticos ya kina Luis Figo, David Beckham, Roberto Carlos na Ronaldo, maisha yake aliamua kuyahamishia Newcastale ndipo akaenda Manchester United.
Lilikuwa tusi kubwa sana alilowatukana mashabiki wa Liverpool, akawa amewasiliti na kujiunga na mahasimu wao wakubwa.
Vilabu hivi mara ya mwisho kuuzia wachezaji moja kwa moja ilikuwa mwaka 1964,mwaka ambao Phil Chisnall alitoka Manchester United kwenda Liverpool.
Tangia hapo hizi timu hazijawahi kuuziana mchezaji moja kwa moja.
Huu ndiyo utakuwa ugumu wa kwanza wa kumpata Henrikh Mkhitaryan , mchezaji ambaye anaonekana hana nafasi katika kikosi cha Manchester United.
Henrikh Mkhitaryan aliwahi kuwa na Jurgen Klopp katika kikosi cha Borrusia Dortmund, wanajuana vizuri hawa wawili.
Henrikh Mkhitaryan anauwezo wa kucheza nyuma ya mshambuliaji, katikati na akitokea pembeni kwenda kwenye box la mpinzani kama alivyo Phillipe Countinho.
Pia ana uwezo mkubwa wa kufunga na kutoa pasi za mwisho za magoli.
Ryad Mahrez.
Ukizungumzia wachezaji ambao walikuwa mhimili wa Leicester City kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya England msimu wa 2015/2016 huwezi acha kumtaja Ryad Mahrez.
Mchezaji bora wa ligi kuu ya England msimu huo wa mwaka 2015/2016. Anauwezo wa kucheza kama Middle Right ( katikati ya uwanja akiwa kulia). Pia anaweza akacheza kama Attacking Middle Right.
Msimu huu amehusika kwenye magoli 14 katika michezo 21 , akiwa ametoa pasi za mwisho za magoli 7 na kufunga goli 7.
Kasi yake, uwezo wake wa kufunga na kutoa pasi za mwisho vinaendana na mfumo wa Jurgen Klopp.
Thomas Lemar.
Kwenye dirisha la majira ya joto Monaco hawakutaka kumwachia.
Lakini hii haimanishi Thomas Lemar ana maisha marefu pale Monaco. Muda wowote anaweza akaondoka.
Na huyu ni moja ya wachezaji ambao wanaweza kuja kuziba nafasi ya Phillipe Countinho.
Ana uwezo wa kucheza kama Attacking Middlefielder kama Phillipe Countinho. Anacheza pia kama Attacking Middlefielder left na Middle Left. Kama nafasi za Phillipe Countinho ambazo huwa anacheza.
Msimu huu kacheza michezo 15 na kahusika katika magoli 6 mpaka sasa.
Manuel Lanzini.
Mzoefu wa ligi kuu ya England kama alivyo Ryad Mahrez.
Ana uwezo wa kucheza nyuma ya mshambuliaji, anauwezo wa kucheza pia kama kiungo wa katikati ( Central Middfielder) na akacheza pia kama Attacking Central Middfielder.
Pamoja na kwamba alikuwa anasumbuliwa na majeraha mpaka sasa amefanikiwa kuhusika katika magoli 6 kwenye mechi 15 alizocheza.
Juan Draxler.
Hana nafasi katika kikosi cha PSG kwa sasa.
Ukiangalia kacheza michezo 13 na kaanza michezo 9 tu msimu huu.
Nafasi yake ni finyu kulingana na kikosi cha PSG kilivyo na nyota wengi kwa sasa.
Kutokuwa na nafasi pana kwake katika kikosi cha PSG kutawapa nafasi kubwa Liverpool ya kumchukua kama wakiamua kumfuatilia kwa ukaribu.