Hii inaweza kuwa ni Habari njema kwa mashabiki na wapenzi wa mabingwa watetezi wa Ligi kuu soka Tanzania bara, Yanga sc, kwa urejeo wa mshambulizi wa kikosi hicho Donald Ngoma.
Ngoma anataraji kuungana na kikosi hicho Alhamisi ya wiki hii, kujiandaa na mchezo wa michuano ya Azam Sports Federation Cup dhidi ya Singida United.
Mmoja wa viongozi wa klabu hiyo, ameiambia tovuti ya Kandanda kuwa kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa daktari zinasema mshambuliaji huyo amepona majeraha yake ya goti.
”Ngoma amepona na ataungana na kikosi Alhamisi, baada ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu na suala la kucheza ni maamuzi ya benchi letu la ufundi ndio wataangalia endapo amekuwa tayari kutumika” alisema kiongozi huyo.
Itakumbukwa mshambuliaji huyo amekuwa nje kwa takribani miezi sita sasa, tangu apate majeraha kunako mchezo wa Ligi kuu bara dhidi ya wakata miwa Mtibwa sugar, mnamo Septemba 30, mwaka jana.
Ngoma anarejea katika kipindi ambacho kikosi hicho kinajiandaa na mchezo wa ASFC, na ule wa mtoano kunako michuano ya kombe la Shirikisho Afrika (CAF) baada ya kuondolea kunako Ligi ya vilabu bingwa Afrika.