Sambaza....

Wananchi wameendelea kujichimbia kileleni mwa Ligi Kuu ya NBC baada ya kuvuna alama zote tatu mbele ya wabishi Geita Gold katika Dimba la Azam Complex.

Licha ya Geita Gold kutangulia kufunga lakini Yanga walitulia na kurudi kwa kasi kipindi cha pili, walirudisha bao hilo na kuongeza mengine na kupata ushindi mnono.

 

Elias Maguli alikua wakwanza kuipa Geita Gold bao baada ya kufunga bao safi kwa kumhadaa mlinzi wa Yanga Dickson Job nakumpiga tobo kipa Djigui Diara na kuukwamisha mpira nyavuni katika dakika ya 20 ya mchezo.

Yanga walirudi kipindi cha pili kwanguvu na kufanikiwa kuandika bao katika dakika ya 48 kupitia Kenedy Musonda alieunganisha kwa kichwa krosi ya Joyce Lomalisa Mutambala. Bao la pili la Yanga lilifuata muda mfupi baada ya Clement Mzize kumalizia mpira uliotemwa na mlinda mlango wa Geita baada ya shuti kali la Musonda.

Jesus Moloko alipigilia msumari wa mwisho kwa Geita katika dakika ya 70 na hivyo kuhitimisha kalamu hiyo ya mabao na kubeba alama zote tatu kutoka kwa Wachimba dhababu.

Kwa ushindi huo sasa Yanga wanaendelea kujichimbia kileleni mwa msimamo kwa kufikisha alama 65 na kuendelea kuiacha Simba kwa alama 8.

Katika mchezo mwingine wa Ligi uliopigwa leo Coastal Union wametoka sare ya bao moja kwa moja na Singida United katika uwanja wa Mkwakwani Tanga. Goli la Coastal lilifungwa na Gerson Gwalala wakati lile la kusawazisha kwa Singida Big Stars lilifungwa na Bright Agyei.

Kwa sare hiyo sasa Coastal wanafikisha alama 26 wakati Singida Big Stars wao wamefikisha alama 47.

Sambaza....