Sambaza....

April 16 imefika na hukumu imetoka bila shida wala tabu yoyote baada ya Wananchi Yanga kukubali kipigo cha mabao mawili kwa sifuri mbele ya Mnyama Simba katika Dimba la Benjamin Mkapa.

Mchezo huo namba tano kwa ubora na ukubwa Barani Afrika ulikua unasubiriwa kwa hamu kubwa na wapenzi wa kandanda nchini hata nje ya nchi kutokana na umuhimu mkubwa wa mchezo huo kwa timu zote mbili za Simba na Yanga.

 

Yanga waliingia katika mchezo huo wakijiamanu mno si tu wachezaji bali hata mashabiki wa Yanga waliingia uwanjani wakijua wanakwenda kumfunga Mnyama kutokana na rekodi nzuri waliyonayo mbele ya Simba katika michezo ya hivi karibuni.

Alikua ni Henock Inonga Baka aliyeanza kupeleka balaa Jangwani na kuwanyamazisha Wananchi katika dakika ya pili baada ya kupiga kichwa safi iliyotokana na krosi ya Shomary Kapombe aliyepokea pasi kutoka kwa Saidoo baada ya kuanziana kona fupi.

Mlinzi wa Simba Henock Inonga Baka akishangilia bao la kwanza la Simba.

Baada ya goli hilo mashabiki wa Yanga walionekana kupoa na kuingiwa na ubaridi uwanjani hapo na pia hali ya hewa ni kama iliwasaliti kwani muda mfupi baada ya bao hilo mvua ilianza na hivyo kuwafanya mashabiki kuloa lakini pia hali ya uwanja ikawa na utelerzi kupoozesha kasi ya mpira.

Dakika ya 32 alikua ni Kibu Denis aliyepeleka kilio tena kwa Wananchi kwa kuandika bao la pili baada ya kupiga shuti kali lililomshinda Djigui Diara mlinda mlango wa Yanga na hivyo kuipelekea Simba mapumziko ikiwa na uongizi wa mabao mawili.

Kibu Denis Prosper akipiga shuti kuandika bao la pili kwa Simba

Kipindi cha pili kilanza kwa Yanga kufanya mabadiliko ya kuwatoa Yanick Bangala, Salum Aboubakar na Jesus Moloko nafasi zao zikichukuliwa na Aziz Ki, Mudathir Yahya na Tuisila Kisinda. Mabadiliko hayo yaliwapa uhai Yanga na kuwafanya kutawala mchezo na kupelekea mashambuli ya hapa na pale lakini mlinda mlango namba tatu wa Simba Ally Salim alikua imara kudaka na kuondo hatari zote langoni mwake.

Kwa upande wa Simba walimtoa Erasto Nyoni nafasi yake ikachukuliwa na Nasorro Kapama, Jean Baleke nafasi yake ilichukuliwa na John Bocco na dakika za majeruhi alitoa Kibu Denis kumpisha Moses Phiri.

Djuma Shabani akipiga hesabu za kumuacha mlinzi wa Simba Joash Onyango.

Mpaka filimbi ya mwisho inapulizwa Simba mbili Yanga hawakupata kitu. Kwa ushindi huo bado Yanga anabaki kileleni akiwa na alama 68 na Simba nafasi ya pili wakiwa na alama 63. 

Wawili hao sasa wanageukia michuano ya Kimataifa ambapo Simba atakua mwenyeji wa Wydad Casablanca siku ya Jumamosi wakati Yanga wao watasafiri kuvaana na Rivers United nchini Nigeria.

Sambaza....