Hatimaye Bernard Morrison ametupa jibu la maswali yetu. Nilikuwa na swali kuhusu ubora wake. Kwanini amefika hapa nchini akiwa na kipaji maridhawa kama chake. Wakati fulani niliwahi kusema ‘ukimuona mchezaji bora sana wa kigeni yupo nchini basi kuna jambo’.
Inawezekana akawa mkorofi na hana nidhamu, inawezekana umri wake umekwenda, inawezekana kuna kitu zaidi ya hayo mambo mawili. Inatokea nadra sana kwa mchezaji wa kigeni anayejielewa kuja kucheza soka nchini na kuacha kwenda katika nchi zenye maslahi makubwa zaidi.
Nilikuwa najiuliza kuhusu Bernard Morrisson kwanini yupo nchini. Nimepata jibu. Ni mchezaji asiyejielewa. Kutojielewa kwake kumemfanya atangetange huku na kule na kushindwa kutulia katika timu moja kwa muda mrefu.
Yanga walimuibua kutoka kijijini kwao Ghana akiwa hana timu. Kwa sasa hainishangazi sana kwanini hakuwa na timu. Mambo anayowafanyia Yanga tulizoea kuyaona kwa wachezaji wa Kitanzania na sio wa kigeni. Lakini yeye amefanya.
Morrison alisaini mkataba mpya na Yanga Machi mwaka huu. Vyanzo vyangu vya uhakika kabisa viliniambia kwamba Morisson alisaini Yanga mkataba mpya wa miaka miwili kwa dau la dola 50,000 na mshahara wa dola 5,000 kwa mwezi.
Yanga walikuwa wamekoshwa na kiwango chake na hawakutaka kumpoteza. Kitu kinachoshangaza kutoka kwake ni namna alivyowageuka. Kuna timu ambayo imemuahidi pesa nono zaidi kuliko ile ambayo Yanga wamempa.
Anachonishangaza ni uswahili wake. Akiwa kama mchezaji anayejitambua sijui kwanini hakusubiri mpaka mkataba wake umalizike ili apime upepo kwa kujiweka kuwa mchezaji huru zaidi. Kwanini hakufanya hivyo na akaamua kukimbilia pesa za wakati huo?
Kwanini aisumbue Yanga sasa? Hili ni swali. Kwanini atake Yanga waufute mkataba wake sasa? Hakujua kama alikuwa ameonyesha kiwango cha kuridhisha mpaka pale alipokaa katika meza na bosi mmoja wa Yanga na kusaini mkataba mpya? Ni swali la kujiuliza.
Lakini mtazame Morisson. Mara nyingi wachezaji wa kigeni huwa wanawakilishwa na mawakala wao katika mazungumzo na timu zao. Mpaka leo hatumjui wakala wa Morrison. Anajiwakilisha mwenyewe tu na ndio maana si ajabu anafanya mambo ya ajabu.
Pamoja na yote tuwakumbushe tu Yanga kwamba wanavuna walichopanda kwa Morisson. Wamemfanya kuwa mkubwa zaidi na mwenyewe ameshtukia. Anawafanya Yanga kuwa mateka wake. Anawashurutisha.
Mchezaji wa kigeni ambaye aligoma kusafiri na timu kwenda Shinyanga na Dodoma bila ya sababu yoyote ya msingi, na bado alipoingia katika pambano dhidi ya Azam akashangiliwa na mashabiki, hapana shaka amegundua kwamba amewakamata mashabiki.
Haishangazi kuona siku chache baadaye akafanya mahojiano na chombo cha habari ndani ya kambi ya klabu yake huku akizungumza habari ambazo si nzuri kuhusu timu yake. Nahisi alikuwa anatafuta sababu wamfukuze.
Yanga pia ni waathirika wa kuwa na timu mbovu na ndio maana Morrison anawasumbua. Kama Yanga wangekuwa na timu kali na yenye mastaa wengi sidhani kama Morrison angewasumbua. Asingewasumbua.
Umuhimu wake ungekuwa sawa na mastaa wengine ndani ya klabu ya Yanga nadhani asingewasumbua. Mkumbuke Emmanuel Okwi wa Simba. Kuna wakati alikuwa mkubwa klabuni kuliko mchezaji mwingine yeyote yule.
Aliwahenyesha sana mashabiki na viongozi. Alikuwa anachelewa kurudi klabuni bila ya sababu ya msingi. Mpaka Simba walipounda timu kabambe kupitia kwa mastaa wengine kama kina Meddie Kagere na John Bocco hapo ndipo Okwi alipopata adabu.
Iliwahi kutokea pia kwa Haruna Niyonzima na Yanga. Kuna wakati aliwahenyesha kwa sababu alikuwa staa mkubwa zaidi klabuni. Baadaye walipotengeneza timu ya akina Thaban Kamusoko alionekana kuanza kutulia klabuni.
Msimu ujao Yanga wakitengeneza timu wanayoifikiria, timu iliyosheheni mastaa, kuna uwezekano mkubwa Morisson akashika adabu. Umuhimu wake utakuwa staa na wengineo. Wachezaji wa Kiafrika wakiwa wakubwa zaidi kuliko klabu huwa wanasumbua.
Hata Ulaya huwa inatokea. Usidhani Lionel Messi na Cristiano Ronaldo ni waungwana sana hapana. Kuna wakati wanaamuru mambo mengi katika timu. Wanaamuru wachezaji wa kucheza nao, wanaamuru wachezaji wa kununuliwa, wanaamuru mambo mengi ndani ya timu. Wakati mwingine wanakuwa na sauti kubwa kuliko makocha.
Chanzo: Eddo Kumwembe.