Sambaza....

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizopata bahati ya kuingiza timu nne katika mashindano ya Caf, Mbili ligi ya  Bingwa na Mbili Shirikisho. Simba na Yanga ndio vilabu vinaiwakilisha nchi katika michuano ya klabu bingwa Afrika na tayari vilabu hivi vimeshacheza mechi za raundi kwanza kabla ya wikiendi hii kukamilisha raundi ya pili katika hatua ya awali ya mashindano hayo.

Yanga ilitoa sare pacha ya goli 1-1 katika uwanja wa taifa, na jumamosi hii watakuwa na kibarua kizito ugenini dhidi ya Township rollers. Rollers ambao wanaonekana kujiamini zaidi, na ukweli ni kwamba Rollers Sio timu ya kitoto.

Township Rollers sio wageni masikioni mwa wadau wa soka. Wadau wengi wa soka nchini wanawajua vizuri tu, na hata aina ya uchezaji wao

Hii ni timu kutoka kwa Wa Makiri kiri Botswana, timu inapatikana pale Gaborone kama maskani yake. Timu hii ina AKA nyingi tu, yaani inafahamika kwa jina la POPA popa, THE BLUES kama Chelsea Vile au Unaweza iita TSE TALA, Pia kama utaaita kwa jina la MAPALASTINA utakuwa hujakosea.

Hii ndio klabu yenye historia kubwa nchini Botswana, hii ndio klabu yenye vikombe vingi vya ligi kuu nchini Botswana na ligi zingine za kitaifa kuliko timu yoyote ile.

Kikosi cha Rollers kinanolewa na kocha Tomas Trucha KUtoka jamhuri ya Czech. Kwa taarifa tu ni kwamba klabu hii si ya kitoto, kwani imeshiriki mashindano ya kimataifa mara 36, na kupata ushindi mara 12, sare 5 na kufungwa 19, maana yake wana uzoefu na michuano ya kimataifa pia.

Ukiachana na mbwembwe hizo za Rollers, Yanga kamwe haiwezi kuwa ‘UnderDog’ katika mchezo huu kwani nayo inahistoria kubwa tu…

Ukiulizwa klabu kongwe zaidi nchini ambayo bado ipo katika ushindani, bila kupepesa macho utaitaja Young Africans. Yanga ndio klabu iliyopo ligi kuu yenye umri mrefu zaidi, ilianzishwa February 11 mwaka 1935.

Yanga ndio klabu yenye mataji mengi zaidi ya ligi kuu Tanzania bara, ndio maana wanaitwa mabingwa wa kihistoria. Wahenga walisema kuwa, ufagio wa zamani unaijua kila kona ya uwanja, umri wa Yanga unatoa msisitizo kwa klabu, wachezaji na wadau wa soka nchini kuwa Yanga ina kila sababu ya kupata matokeo ugenini na hata nyumbani.

Acha nikusogezee sababu 5 za kwanini Yanga ina kila sababu ya kupata matokeo ugenini. Kwa maana nyingine, kupitia sababu hizi yanga wasipopata matokeo mbele ya Rollers watakuwa wamefanya makusudi.

1. KUSAFIRI MAPEMA.

Yanga ilisafiri tangu Jumatatu kuelekea nchini Botswana kupitia Afrika Ya kusini. Kwa mahesabu ya haraka haraka, Yanga itakuwa na Siku 5 za maandalizi kabla ya siku ya mechi.

Kusafiri mapema kuna maida nyingi kwa klabu, kwanza ni kuzoea hali ya hewa ya eneo husika, pili kuepusha uchovu wa safari siku ya mechi, yaani huwapa wachezaji na benchi la ufundi kupata mapumziko zaidi, tatu ni kujua mazingira ya ugenini kwa upande wa vyakula, sehemu pa kulala na sehemu ya kufanyia mazoezi.

Kwakuwa Yanga wamewahi mapema, hakutokuwa visingizio vya uchovu wa safari wala ugeni wa mazingira.

Kusafiri mapema pia kunaisaidia Yanga kukwepa hujuma za wenyeji wao. Soka la Afrika lina njia zake za kupita, kwenda mapema maana yake watakuwa wamejiandaa vizuri kwa upande wa vyakula na mahitaji mengine bila kuwategemea wenyeji wao.

2. HALI YA KIKOSI NA MORALI YA TIMU.

Baada ya kupata ushindi katika mchezo wa kirafiki dhidi ya FC Leopard, Morari ya Yanga imepanda haraka na kuwa kubwa. Morali hii itaisadia klabu kupata matokeo chanya ukizingatia matokeo ya mechi hiyo ni hatma ya Yanga katika michuano ya kimataifa.

Msimu uliopita Yanga ilihaha kuwa na straika mwenye uwezo wa kufunga sawa na Heritier Mkambo, lakini msimu huu mambo ni Super yaani kuna kila aina ya wachezaji yaani hapa kuna Patrick Sibomana, Isa Bigilimana, Winston Kalengo,Sadney Ukhrob, Juma Balinya, Mapinduzi Balama, Mustapha Selemani, Lamine Moro na wengine kibao ambao tayari wameshaonyesha cheche zao.

Kikosi hiki kinadaiwa kukosa muunganiko, lakin hata hivyo kwa mchezo walioucheza kipindi cha pili katika mechi ya awali dhidi ya Rollers ni dalili kuwa kikosi hiki ni kizima na chenye afya tele.

3.MASLAHI YA NCHI.

Yanga ni ya Tanzania, Yanga sio ya Mshindo Msolla au Dismas Ten. Yanga huiwakilisha Tanzania yenye zaidi ya watu  milioni 50.

Ushindi wa Yanga utainufaisha nchi kuendelea kuingiza timu 4 katika mashindano ya Afrika. Kwa sasa Tanzania imepata nafasi hii baada ya kujikusanyia alama 18 ikiwa katika nafasi ya mwisho ya 12 katika msimamo wa timu 12 zinazotakiwa kuingiza timu 4 katika mashindano ya Caf.

Msimamo huu unamaanisha kuwa, Yanga au Timu yoyote ya Tanzania ikiteleza, kutazipa nafasi nchi zingine kuipita Tanzania kialama na mwishowe Tanzania Kutupwa nje ya 12 bora na kukosa fursa ya kuingiza timu nne.

4. KOCHA MWINYI ZAHERA.

Wangapi wanamuamini kocha Mwinyi Zahera? Wangapi wanaamini kama Zahera ni bonge la kocha? unamuamini zahera au la!

Kwa leo sitamuongelea kiufundi, lakini namtazama kocha Zahera katika mlango mwingine usionekana. Mlango ambao unapatikana ndani ya Zahera mwenyewe na wala sio kufuata hatua za kisayansi au kiintelijensia.

Zahera anajua jinsi ya kuwaandaa wachezaji kisaikolojia. Saikolojia ndio kila kitu kwa mchezaji. Katika hili kuna kitu kinaitwa Law of attraction kwa maana kile unachokifikia, na kukiweka moyoni na akilini kwa muda mrefu huwa kinatokea kama unavyowaza.

Vivyo hivyo, Zahera anauwezo wa kuwaandaa kisaikolojia wachezaji wake waamini kuwa wanaweza kupata matokeo ugenini. Kama aliweza kushika nafasi ya pili ligi kuu Tanzania bara msimu uliopita licha ya njaa kali Jangwani atashindwaje kuwatia ukichaa wachezaji wake kucheza jihad dhidi ya Rollers? it is possible!

5. REKODI NA ASILI YA HATUA YA AWALI YA MASHINDANO.

Katika msimu uliopita kuna vilabu kadhaa ambavyo vilipata sare nyumbani na ugenini bado vikapata matokeo. Township Rollers wenyewe walipata Sare nyumbani ya 1-1 dhidi ya Bantu na ugenini nako wakapata sare kama hiyo, wakapita kwa njia ya matuta.

Kwa maana hiyo, katika hatua hii ya awali timu nyingi huwa ni za kawaida na zinafungika popote pale.

Pili, Uhitaji wa Yanga katika mechi hiyo ni ushindi, ushindi ambao unaweza kuwa wa goli moja na kuendelea, kwa maana hiyo kirahisi kabisa unaweza sema Yanga inahitaji goli 1 tu na kutoruhusu milango yake kuguswa. Je itawezekana?

Unaikumbuka Manchester United mwaka huu ligi ya mAabingwa ulaya hatua ya 16 bora? Mechi ya kwanza Man U walikubali kichapo cha goli 2-0 nyumabni dhidi ya PSG.. watu wengi walijua ndio mwisho wa kikossi kibovu cha Man U chini ya Ole Gunnar, lakini kilichowakuta PSG kwao kiliwashangaza wengi. Man Ulishinda 3-1.

Tatu, Takwimu za Soka na mtazamo wa makocha na wachezaji juu mechi za ugenini unabadilika kila kukicha, Zamani ilikuwa ni ngumu kupata matokeo ugenini lakini siku hizi ni rahisi sana,

Mfano katika ligi kuu nchini Uingereza- epl asilimia 38.5% pekee timu zimepata matokeo nyumbani lakini asilimia zilizosalia, ni ushindi wa ugenini, hii ina maana kuwa faida ya uwanja wa nyumbani inazidi kupungua kila kukicha.

Nikirudi Afrika, utabaini kuwa, timu nyingi hazina uwezo wa kuzitumia vyema faida za uwanja nyumbani hasa katika kuwakusanya mashabiki wake na kuwajaza uwanjani na kuwashangilia.

Viwanja vya Afrika huwa havina watazamaji wengi kiasi cha kuwatisha wageni. Yanga imezoea kucheza viwanja vya ugenini vyenye mashabiki waliojaa mpaka pomoni ligi kuu, hivyo si rahisi kutishwa na idadi kiduchu wa mashabiki wa Rollers.

Kwa sababu hizi Yanga inawabidi washinde mechi hii. Kwa sasa wanahitaji kuwaweka sawa wachezaji kisaikolojia, pili ni kocha Zahera kuhakikisha anaisoma vyema Rollers na kuja na mpango kazi wenye kutekelezeka uwanjani, tatu wachezaji, benchi la ufundi wanatakiwa kuwa wavumilivu ndani ya uwanja, hata ikitokea wakaanza kufungwa isiwe sababu ya kukata tama, nne ni kujitahidi kukwepa hujuma za wenyeji na Tano, Yanga kwa sasa inahitaji dua za Watanzania..

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Yanga.

Sambaza....