Kuna wakati Yanga walimwihitaji sana Emmanuel Okwi. Uzuri ni kwamba wakati huo ndiyo ulikuwa wakati ambao Yanga wangefanya chochote bila klabu yoyote kuizuia Yanga.
Ndiyo wakati ambao hata wapinzani wao wakubwa Simba walikuwa wanyonge mbele yao. Ndiyo wakati ambao Yusuph Manji alikuwa na mikono imara ambayo ilikuwa inatisha sana.
Mikono ambayo ilikuwa na uwezo wa kuchukua chochote na kwenda nacho popote. Hii ilikuwa mikono ya pesa. Mikono ambayo ilifanikisha kununua penzi la Emmanuel Okwi.
Penzi ambalo lilionekana tamu katika mitaa ya msimbazi. Yanga walilitamani penzi lile, wakatamani kuwa halo hata kwa dakika moja, walifanikiwa kwenye hilo.
Walimleta Emmanuel Okwi katika mitaa ya jangwani. Kwao wao walikuwa wanataka penzi. Ilikuwa ngumu kwao wao kununua moyo wa Emmanuel Okwi Lakini ilikuwa vyepesi sana kwao wao kununua penzi lake.
Walifanikiwa kwenye penzi , wakashindwa kwenye moyo . Mwili ulikuwa jangwani Lakini moyo ulikuwepo Msimbazi , sehemu ambayo penzi lake la dhati lilipo. Hakuweza kucheza kwa moyo akiwa na jezi ya njano.
Kwake yeye jezi nyekundu ndiyo iliyokuwa inampa moyo wa kucheza kwa moyo. Mwisho wa siku hakufanya vizuri akiwa na jezi ya Yanga. Yanga ilihitaji moyo wa Emmanuel Okwi ili wafurahie mafanikio yake, Lakini kwa bahati mbaya moyo wa Emmanuel Okwi ilikuwa mbali na nyumba ya Yanga.
Miaka mingi imepita , hatimaye Leo Yanga wamempa Emmanuel Okwi sahihi . Emmanuel Okwi ambaye anauwezo mkubwa kama ule uwezo wa Emmanuel Okwi wa kipindi cha Yusuph Manji.
Na bahati nzuri Emmanuel Okwi huyu wa sasa ana mapenzi ya dhati na Yanga , anacheza kwa moyo akiwa na timu ya wananchi ndiyo maana anawasaidia sana. Leo hii katika mechi mbili amefunga goli moja na pasi tatu za mwisho zilizozaa goli.
Inawezekana kwa kipindi kile ilikuwa ngumu sana kuvipata vyote kwa Emmanuel Okwi yani penzi pamoja na moyo wenye mapenzi ya dhati na Yanga Lakini kipindi hiki Emmanuel Okwi narudi na vyote viwili , Lakini karudi katika sura ya Bernad Morrison.