Sambaza....

Mchezo wa kwanza wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika umemalizika kwa Yanga kupoteza kwa mabao mawili kwa moja mbele ya wageni wao USM Algiers katika Dimba la Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam.

Mvua kubwa iliyoanza kunyesha tangu asubuhi ulionekana kuathiri mchezo huo kwa kiasi kikubwa kwani uwanja ulijaa maji na kuufanya uwe unateleza na kuwapa tabu wachezaji wa timu zote mbili haswa kipindi chakwanza.

Katika mchezo huo wageni Algiers ndio waliokua wakwanza kupata bao ambapo katika dakika ya 32 Ahmen Mahious aliitanguliza timu yake kwa mpira wa kichwa akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa baada ya Dickson Job kufanya madhambi.

Wachezaji wa USM Algier wakishangilia goli.

Kipindi cha pili Yanga walisawazisha katika dakika ya 82 kupitia kwa Fiston Mayele ambae leo amefikisha mabao saba katika michuano hiyo na kumpiku Rango Chivaviro mwenye mabao sita.

Haikupita muda sana dakika ya 84 tena Algiers waliandika bao kupitia kwa Islam Merili aliemalizia kazi nzuri iliyofanywa na winga msumbufu Bousseliou na kuufanya mchezo huo kumalizika kwa Yanga kupoteza kwa mabao mawili kwa moja.

Wananchi sasa wana kibarua kigumu chakupindua matokeo katika mchezo wa fainali ya pili utakaopigwa Jijini Algiers nchini Algeria siku ya June 3 yaani wiki moja baada ya mchezo wa leo.

 

Sambaza....