Sambaza....

Msafara wa wachezaji na viongozi wa klabu ya Yanga umefanikiwa kufika nchini Congo DR licha ya kuchelewa kuondoka nchini Tanzania kutokana na matatizo ya kiufundi ya ndege.

Kikosi cha Yanga kilipaswa kuondoka nchini Alhamisi ya jana asubuhi majira ya saa tano lakini walikwama kuondoka huku safari hiyo ikikwama na kusogezwa masaa mbele.

 

Yanga wakiwa uwanja wa ndege wa Julius Kambarage Nyerere walishuhudia safari yao ikisogezwa mbele zaidi ya mara mbili na mpaka wanaanza safari ilikua ni majira ya saa tatu usiku hivyo kusubiri safari hiyo kwa takribani masaa 12 uwanjani hapo.

Wananchi hatimae walifika nchini Congo DR kwenye majira ya saa nane usiku kwa saa za Tanzania na msafara mzima wa wachezaji na viongozi kuelekea moja kwa moja hotelini kupumzika.

Yanga wapo nchini humo kuelekea kumaliza ratiba ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe mchezo utakaopigwa siku ya Jumapili saa kumi jioni.

Fiston Mayele akimuacha mlinzi wa TP Mazembe katika mchezo wa kwanza Jijini Dar es salaam.

Kuelekea mchezo huo ambao Yanga wanaongoza kundi D tayari Wananchi wanauchukulia kwa umuhimu mchezo huo na wakijiapiza kutaka kuweka rekodi nzuri ya kumaliza wakiwa vinara wa kundi lao.

Kama Yanga watafanikiwa kuongoza kundi lao mbele ya Watunisia US Monastir itakua ni mara yao ya kwanza kwani tangu waliposhiriki hatua hiyo ya makundi mara mbili hawakuwahi kuwa si tu vinara lakini pia kuvuka hatua hiyo ya makundi.

 

Sambaza....