Safari ilianzia kwenye kipaza sauti cha Yanga, yeye ndiye aliyetakiwa kukichukua na kukisogeza karibu na mdomo wake kwa ajili ya kuisemea Yanga. Jukumu la kujenga picha nzuri ya Yanga lilikuwa lake.
Jukumu la kuitetea Yanga lilikuwa lake chini ya mwamvuli wa Afisa Habari wa Yanga. Cheo ambacho wana Yanga wengi walikuwa wametoka kuleweshwa na Jerry Muro.
Huyu alikuwa anaiongea sana Yanga kwa mazuri , na alipogeuka upande wa pili aliisema vibaya sana Simba mpaka Simba wakawa wanyonge , kipindi cha Jerry Muro ndicho kipindi ambacho Simba walikuwa wanyonge sana.
Ndicho kipindi ambacho hata Haji Manara huyu anayetamba muda alikuwa mdogo sana kwa Jerry Muro , sawa kulikuwa na vita kali kati ya hawa wawili lakini mfalme wa vita alikuwa Jerry Muro.
Aliwanyanyasa sana Simba, alimnyanyasa sana Haji Manara, Haji hakuwa na amani, kila alipokuwa anapita sauti moja ya Jerry Muro ilikuwa inapita sikioni mwake ikisema wewe ni wa mchangani.
Ndicho kipindi ambacho wana Yanga walikuwa wanatembea kifua mbele, lakini ghafla zama hizi zilianguka ghafla tena Baada ya Yusuph Manji kuondoka kwenye klabu hii.
Nguvu ya Jerry Muro ikaisha na yeye akaamua kukaa pembeni , akawa anasubiriwa mtu ambaye atasimama kuziba nafasi yake , kwa bahati Mbaya Dismass Ten ndiye aliyekuwa mtu wa kuziba pengo lake.
Nimetumia neno bahati mbaya kwa sababu Dismass Ten hakuwa na tabia kama za Jerry Muro , tabia za kusema sana. Tabia za kunanga sana , yeye mdomo wake ulikuwa mzito sana.
Mdomo wake ulikuwa siyo wa kuwafurahisha mashabiki wa Yanga , yeye alijaribu kuibadilisha Yanga kwenye kitengo cha Habari. Alijaribu kukiweka kitengo hiki kiwe cha kisasa zaidi yani kiendeshwe kulingana na mahitaji ya sasa.
Kipindi chake kukawa na mabadiliko ya utoaji wa Habari , kipindi chake kukawa na Yanga TV lakini vyote hivi mashabiki wa Yanga walikuwa hawavioni , wao walikuwa wanataka yeye aiseme vibaya Simba tu.
Hawakupenda kumuona Haji Manara alivyokuwa anatamba, walitaka yeye ashindane na Haji Manara , kwa bahati Mbaya Dismass Ten ni mtu wa Mbeya na Haji Manara ni mzaramo!.
Tarataibu wakaanza kumwamisha vitengo Dismass Ten Baada ya kuonekana anashindwa kabisa kupambana na Haji Manara. Alianza safari ya kukaimu vitengo.
Mara kaimu karibu mkuu, mara kaimu Afisa masoko , mara akapelekwa kuwa Kaimu Meneja wa Yanga. Hapa ndipo aliponasa ndoano. Ndoano ambayo alikuwa ametengewa kwa muda mrefu.
Sitetei kosa alilolifanya , kosa la kuwavisha benchi la ufundi mavazi ambayo siyo rasmi na yale yanayozalishwa na GSM. Sijui kosa lilianzia wapi na yupi mwenye kosa , lakini adhabu hii imekuja Baada ya Yanga kuchoka kuishi na Dismass Ten !