Sambaza....

Kuna mengi ya kujifunza kwenye kichwa cha Mwinyi Zahera, kinywa ambacho mara nyingi ni faida kukipa sikio lako.

Kinywa ambacho kinaonekana kina mengi ya kiufundi cha kutoa, lakini ndicho kinywa ambacho kiliwapa nguvu Yanga.

Hawana nguvu ya pesa ya kupigana kama misimu kadhaa iliyopita. Hawana nguvu ya wachezaji wengi bora kama kipindi cha nyuma.

Kipindi ambacho kikosi chao kilikuwa kimeundwa na wimbi la wachezaji bora sana. Wachezaji ambao walikuwa wanaisaidia sana Yanga.

Hakuna kocha ambaye asingetamani kuwa na wachezaji kama Donald Ngoma, Simon Msuva, Obrey Chirwa, Kamusoko, Haruna Niyonzima kwa wakati mmoja.

Ni wachezaji ambao wanaweza kukuhakikishia ushindi muda wowote, ndiyo wachezaji ambao walikuwa na vipaji vya hali ya juu.

Kwa sasa hali ni tofauti kabisa. Yanga haina wachezaji wengi wenye vipaji vikubwa ndani ya timu kama kipindi cha nyuma.

Haina tena huduma bora za kifedha kama kipindi cha nyuma. Wapo tu , wanaunganisha timu yao. Na mtu pekee ambaye anaiunganisha timu ni kocha wao.

Mwinyi Zahera anaonekana kuwa mtu muhimu sana katika kikosi cha Yanga. Ameifanya Yanga iongoze ligi mpaka sasa tena katika mazingira magumu.

Ajib

Ameifanya Yanga irudishe kujiamini kwake bila hata kutumia pesa nyingi kama kipindi cha nyuma ambapo walikuwa wanapata huduma bora.

Amewafanya wachezaji watamani kucheza mpira kwa ushindani na kupata matokeo chanya bila kujalisha hali ambayo wanapitia.

Huyu ndiye Mwinyi Zahera, ambaye aliwafanya mpaka Yanga wasahau kuwa kuna kufungwa tena kwenye ligi kuu ya Tanzania bara.

Ilifikia wakati kuanzia mashabiki wa Yanga waliamini kuwa timu yao itamaliza ligi bila kufungwa na hii ni kwa sababu ya Mwinyi Zahera.

Na mwisho wa siku hii imekuja kuwa na madhara kwa timu. Jana wamepoteza dhidi ya Stand United. Ikiwa ni mchezo wao wa kwanza kupoteza.

Kipigo ambacho hawakutegemea kutokea. Kwao wao walikuwa wanaamini kabisa watamaliza dakika 90 bila kufungwa.

Kujiamini kulikuwa kumeongezeka sana kwa wachezaji wa Yanga na mashabiki wa Yanga. Wao waliamini ushindi waliumbiwa wao.

Wao ndiyo walikuwa na hatimiliki ya ushindi, wao ndiyo walikuwa na haki zote za kupata ushindi kuliko timu yoyote ile kwenye ligi kuu Tanzania bara.

Ndiyo maana hata kwenye mchezo wa jana wachezaji wa Yanga waliingia kwa kujiamini saña kupita kawaida. Nyuso zao zilionesha kujiamini kwao kwa hali ya juu.

Ndiyo maana hata walipokuwa wanacheza hawakuwa na ile hamu kubwa ya kushinda hiyo mechi kwa sababu tu ya kujiamini sana.

Hawakuwa makini sana na maamuzi yao ndani ya uwanja. Nidhamu ya kufanya maamuzi ilikuwa finyu sana jana kwa sababu tu ya kujiamini sana.

Kitu ambacho kiliwapelekea Stand United kutulia na kuwaadhibu Yanga. Adhabu ambayo ni faida kubwa sana kwa Yanga.

Adhabu ambayo imewakumbusha Yanga kuwa hawatakiwi kujiamini kupitiliza mpaka kusahau kuwa hii ni ligi.

Ligi ambayo kila mtu anaweza kushinda, ligi ambayo inaushindani mkubwa. Kwa kipigo cha jana kimewakumbusha ushindani huu.

Kimewakumbusha kuwa wao hawana hatimiliki ya kushinda, kimewakumbusha kuwa wao wanatakiwa kuendelea kupigania ubingwa.

Kimewakunbusha kuwa kuna umuhimu wa kumheshimu kila mpinzani ambaye atakutana naye kwenye ligi kuu ya Tanzania bara.

Sambaza....