Ile picha ambayo haikuwepo vichwani mwa watu wengi , ndiyo ile picha ambayo ilianza kuchorwa pale Serena Hotel. Hotel yenye hadhi kubwa sana kimataifa , nyota tano ndiyo hadhi ya hotel hii.
Hapa ndipo safari ya kuchora ile picha ya Yanga ilipoanzia. Picha hii inachorwa kwa wino wa matumaini , wino ambao umejaa tabasamu kubwa sana kwa wana Yanga , tabasamu ambalo lina matumaini ya kuwa kesho yao ni bora .
Kesho ambayo imeandikwa kwenye makaratasi ya GSM , Yanga na La Liga . Makaratasi ambayo yanaipa nafasi kubwa sana Yanga kukimbia kuelekea katika sehemu ya mabadiliko ya uendeshaji wa klabu kwa kuendana na mazingira ya kisasa ya mpira wa miguu.
Jambo jema sana , jambo ambalo ni kubwa sana , jambo ambalo Yanga SC wanastahili pongezi nyingi kuliko kuwa na mashaka nao kuhusiana na mchakato huu wa mabadiliko ya uendeshaji wa mpira wa miguu ndani ya klabu yao.
Kwanza kitendo cha wao kutaka kufanya mabadiliko ndicho kitendo cha kwanza ambacho wanatakiwa kupongezwa . Ni hatua ambayo kwa miaka mingi tumekuwa tukiwapigia kelele waanze kuipiga lakini hawakuwahi kutusikia.
Hata kipindi ambacho walijarubu kutaka kufanya mabadiliko ya kiundeshaji ndani ya klabu walirudi nyuma tena baada ya hatua yao ya kwanza ya mabadiliko. Macho yangu yashawahi kushuhudia mabadiliko ya Yusuph Manji yakishindwa kutekelezwa.
Wanachama waliunda makundi mawili , wapo waliokubaliana na mtazamo wa mwenyekiti wao Yusuph Manji na wapo ambao hawakukubaliana na mtazamo wa mwenyekiti wao Yusuph Manji , kukawa na makundi mawili. Lile kundi linakubaliana na mwenyekiti na lile kundi ambalo lilikuwa linampinga mwenyekiti.
Mwisho wa siku hakuna kitu ambacho kilifanikiwa kwenye hili kama ambavyo ilivyokuwa kwa Yanga Kampuni na Yanga asili. Mwenyekiti alitamani Yanga iendeshwe kama kampuni lakini kuna kikundi cha watu kilikataa na kujiita kuwa no Yanga asili . Mchakato wa mabadiliko ukaishia hapo.
Huu ni mchakato wa tatu , mchakato ambao naamini umeanza baada ya uongozi wa Yanga kujifunza kutoka kwenye michakato iliyopita , naamini wanajua ni wapi ambapo michakato mingine ilikwama na nina amini kwa sasa wako tayari kuhakikisha mchakato huu haukwami.
Ndiyo maana wamemuomba La Liga awe mshauri mkubwa wa aina ya gani ya uendeshaji wa timu unafaa kwa manufaa makubwa ya Yanga . La Liga ni chombo ambacho kimefanikiwa sana kwenye soka la kisasa , ni chombo ambacho kinajua vyema biashara ya mpira wa miguu.
Ni chombo ambacho kinajua namna ya kuendesha mpira kwa faida . GSM kuisaidia Yanga kulipa gharama ya ushauri kwa La Liga ni kitu kikubwa ambacho Yanga wanatakiwa wakae chini na kutumia kama nafasi kubwa ambayo wameipata.
Nafasi ambayo haitovurugwa na kama michakato mingine ilivyovurugwa . Mimi sina tatizo na La Liga , sina tatizo na GSM wala sina tatizo na Yanga . Tatizo langu liko kwa wana Yanga wenyewe . Yapi matamanio yao ?
Matamanio yao ni kuendelea kuona ikiifunga Simba huku wakifanya vibaya kwenye michuano ya kimataifa ? Sidhani kama haya ndiyo matamanio yao, siamini kwenye hilo na kama ni matamanio yao ningewaomba watamani kwenye hili eneo.
Wautazame uwanja wa Kigamboni ambao walipewa na mheshimiwa mkuu wa mkoa , Paul Makonda. Wafikirie picha ya kituo kikubwa cha kuibua , kukuza na kulea vijana wenye vipaji vya mpira wa miguu. Wakitazame kituo hicho kwa jicho kubwa .
Kituo ambacho kitawawezesha wao kuwa na timu imara , kituo ambacho kitawawezesha wao kuwa na mauzo makubwa ya wachezaji nje ya nchi na kizuri zaidi kwenye mkataba huu na La Liga , Sevilla ni timu rafiki kwa Yanga . Ni vizuri urafiki huu udumishwe kwa Yanga kuwa na kituo hiki cha kuibua , kulea na kukuza vipaji.
Kituo ambacho Sevilla wataleta wataalamu wao kwa ajili ya kunishindisha watoto hawa na baadhi ya makocha wa timu za vijana za Yanga, Sevilla watajaribu kuchukua wachezaji wenye vipaji kwenye kituo hiki na kuvipeleka kwao kwa ajili ya kuviendeleza zaidi .
Natamani wanaYanga kwa sasa wafikirie hivo, wafikirie pia namna gani ambavyo wataweza kushindana na timu kubwa barani Afrika kama Tp Mazembe , Zamaleki na Al Ahly.
Kuyafikia yote haya ni lazima kuwepo na mabadiliko ya dhati ya mfumo wa uendeshaji wa klabu , mfumo ambao utaruhusu Yanga kuendeshwa kama bidhaa kubwa , bidhaa ambayo itaweza kushindana mpaka ndani ya uwanja.
Kama watakosa nafasi ya makubaliano ya namna ya uendeshwaji wa klabu yao basi watakuwa wanaendelea kuwaza namna ya kushindana na Simba SC na siyo kushindana na timu kubwa barani Afrika ambazo zimewekeza sana. Mabadiliko haya yaje na mawazo ya kushinda vikombe vya CAF na siyo vya TFF.